Kwa mujibu wa tovuti ya levif, kamishna huyo amesema baadhi ya nchi wananchama wa Umoja huo wamekuwa wakikandamiza na kukanyaga haki za Waislamu kwa kutunga sheria zinazowakandamiza na kuwawekea vikwazo vingi.
Amesema nchi kama vile Ufaransa na Ubelgiji mwaka uliopita wa 2011 zilitunga na kupitisha sheria zinazowabana wanawake wa Kiislamu wanaovalia vazi la stara la hijabu na hivyo kuwaadhibu wanapovalia vazi hilo hadharani. Vilevile nchini Italia kuna sheria ya zamani ambayo inapiga marufuku wanawake wa Kiislamu kufunika nyuso zao kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, jambo ambalo limepelekea wanawake wengi wa Kiislamu kutiwa mbaroni na maafisa wa usalama.
Amesema katika sehemu nyingine ya ripoti yake kwamba kupigwa marufuku ujenzi wa minara ya misikiti nchini Uswisi mwaka 2009 ni mfano mwingine wa dhulma na ubaguzi unaofanywa dhidi ya Waislamu barani Ulaya. Amesema, vyama vya kisiasa barani Ulaya hufanya kampeni za kujizolea kura za Waislamu na hatimaye kutumia kura hizo kutunga sheria zinazokiuka wazi haki zao.
Amezitaka nchi za Ulaya na hasa Bulgaria kuondoa sheria hizo za kibaguzi dhidi ya Waislamu kwa sababu wao ni sehemu ya jamii za nchi hizo na ambao wana haki ya kulindwa na kuheshimiwa haki zao kama wanachi wengine wa nchi hizo. 1062231