Baada ya Khalid Mash'al, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kutembelea Cairo wiki iliyopita na kuonana na Rais Muhammad Mursi wa Misri, juzi Jumatano, Waziri Mkuu wa Palestina, Ismail Haniya naye alitembelea Misri na kuonana na Rais Mursi, jambo ambalo linaonesha wazi kuanza kipindi kipya cha uhusiano kati Misri na Palestina.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Mursi kuonana na Waziri Mkuu wa Palestina, Ismail Hania, tangu alipoapishwa kuwa rais wa Misri. Katika mazungumzo yaliyofanyika Alkhamisi iliyopita kati ya Mursi na Khalid Mash'al; mkuu huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas alimpongeza Muhammad Mursi kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Misri na kusema kuwa, kuingia madarakani Rais Mursi huko Misri ni sawa na kuanza kipindi kipya cha uhusiano wa nchi hiyo na Palestina. Wakati wa utawala wa dikteta Hosni Mubarak, Misri ilifuata siasa zilizokwenda kinyume na matakwa ya wananchi dhidi ya taifa la Palestina. Utawala wa dikteta Hosni Mubarak ulikuwa muungaji mkono wa pande zote wa utawala wa Kizayuni ambao mikono yake imejaa damu za Wapalestina wasio na hatia. Si hayo tu, lakini utawala wa dikteta Hosni Mubarak uliupatia utawala wa Kizayuni wa Israel gesi ya Misri kwa bei ya kutupa, huku wananchi wa Misri wakiteseka kwa kukosa gesi ya kutumia majumbani mwao. Vile vile dikteta Mubarak alifunga kivuko cha Rafah ambayo ndiyo njia pekee waliyobakishiwa Wapalestina ya kutoka nje ya Ukanda wa Ghaza, na wakati Wapalestina hao walipolazimika kuchimba njia za chini ya ardhi ili kujiokoa na mateso, dikteta Mubarak aliamua kujenga ukuta wa chuma wenye kina kirefu chini ya ardhi ili kuwazuia Wapalestina hao wasitoke nje ya eneo la Ghaza lililozingirwa kila upande. Mambo hayo yaliwakasirisha mno wananchi wa Misri na yanahesabiwa kuwa ni miongoni mwa sababu zilizowafanya wananchi hao waamue kumpindua dikteta Mubarak. Utawala wa Kizayuni aidha unaungwa mkono pia na tawala kadhaa za kidikteta za nchi za Kiarabu kama ambavyo una uungaji mkono wa kila upande kutoka kwa nchi za Magharibi. Sasa kuchaguliwa Muhammad Mursi kuwa rais mpya wa Misri, rais ambaye anatangaza waziwazi uungaji mkono wake kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina, ni sawa na kufunguliwa ukurasa mpya katika uhusiano wa mataifa hayo mawili ya Kiislamu, yaani Misri na Palestina. Ni hivi majuzi tu ambapo Misri ilitangaza kuwaondolea viza wananchi wa Palestina wanaoingia Misri. Inatarajiwa kuwa, taifa la Misri sasa litaweza kutekeleza majukumu yake na kutoa mchango unaotakiwa kwa ajili ya ukombozi wa Quds tukufu na kuwaunga mkono wananchi madhlumu wa Palestina, na kwa kweli hakutarajiwi kitu kingine kutoka kwa wananchi Waislamu wa Misri, ghairi ya jambo hilo.
1063301