Kwa mujibu wa tovuti ya Islamenfrance, Waislamu hao wamechukua hatua hiyo kupitia tangazo walilotoa kupitia mtandao wa intaneti na kama alama ya kulalamikia kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana na mauaji hayo ya kinyama yanayotekelezwa dhidi ya raia wasio na hatia.
Taarifa iliyotolewa na Waislamu hao inasema kuwa ni jukumu na wadhifa wa kidini wa kila Mwislamu kusikia na kujibu kilio cha Mwislamu mwenzake. Imesema Waislamu wa Ubelgiji wamechukua uamuzi wa kufanya maandamano hayo kwa lengo la kujibu wito huo muhimu wa Kiislamu na pia kulalamikia kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana na mauaji hayo dhidi ya jamii ya Waislamu wa Myanmar.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba maandamano hayo yamepangwa kuanza saa 9 alasiri mbele ya ubalozi huo na kwamba tayari vibali vya kuyaruhusu vimechukuliwa kutoka kwa vyombo husika.
Waislamu wa Ubelgiji wanasema wamesikitishwa na ukweli kwamba licha ya kufanyika mauaji ya kinyama dhidi ya watu wasio na hatia huko Myanmar, lakini mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel wa nchi hiyo hajatamka hata neno moja la kuyalaani na kwamba amekaa kimya pembeni ya jamii ya kimataifa akishuhudia mauaji ya umati yakifanyika dhidi ya Waislamu wanaoishi katika mkoa wa Rakhine. 1068442