Mkutano huo ulifunguliwa kwa wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu na kiraa ya Qur’ani Tukufu.
Viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi 120 wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote wako hapa Tehran ambako mbali na kuchunguza na kupasisha hati ya mkutano wa 16 wa jumuiya ya NAM wanaeleza misimamo yao kuhusu masuala mbalimbali ya kieneo na kimataifa na njia za kimatendo za kutatua matatizo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mkutano wa NAM hapa mjini Tehran ulianza Jumapili iliyopita katika kiwango cha wataalamu wa ngazi za juu kwa kaulimbiu ya “Amani ya Kudumu Chini ya Kivuli cha Uongozi wa Pamoja wa Dunia” na walichunguza na kupasisha hati ya mkutano wa 16 wa NAM katika kamisheni mbili za masuala ya kisiasa-kiuchumi na kijamii na kutayarisha rasimu ambayo baadaye ilipasishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa jumuiya ya NAM.
Miongoni mwa nukta muhimu za mkutano wa sasa wa NAM ni kukubaliwa uanachama wa Jamhui ya Azerbaijan na Fiji na wawakilishi wa nchi hizo wameshiriki kwa mara ya kwanza katika vikao vya NAM.
Mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika NAM ambao umeanza mapema leo utaendelea kwa kipindi cha siku mbili baada ya kufunguliwa ka hotuba ya Imam Ali Khamenei na baada yake Rais Muhammad Mursi wa Misri alitoa ripoti kuhusu utendaji wa jumuiya hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya uenyekiti wa Misri katika jumuiya hiyo. Baada ya hapo Rais Ahmadinejad alihutubia kama mwenyekiti mpya wa Jumuiya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote.
Miongoni mwa wageni walikwa katika mkutano huu ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi yaa Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika mkutano wa viongozi wa NAM itawajieni hapo baadaye. 1087880