IQNA

Karii wa Iran aibuka mshindi mashindano ya kimataifa ya Qur’ani Tunisia

14:18 - September 05, 2012
Habari ID: 2405877
Karii wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameshika nafasi ya kwanza katika sehemu ya kiraa ya mashindano ya kimataifa ya hifdhi na kiraa ya Qur’ani ya Tunisia.
Sherehe ya kuhitimisha mashindano hayo ya kimataifa ilifanyika jana katika ikulu ya Rais wa Tunisia Munsif al Marzuqi ambapo washindi wa tano wa kwanza wa hifdhi na kiraa walitangazwa.
Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ramadhaani Gol amesema Hassan Danesh, mwakilishi wa Iran alishika nafasi ya kwanza katika kiraa ya Qur’ani akifuatiwa na Jamal al Umari kutoka Misri aliyeshika nafasi ya pili na Yusuf Abdul Haqq kutoka Yemen ambaye ameshika nafasi ya tatu.
Katika mashindano ya hifdhi ya Qur’ani nzima Muhammad al Atrash kutoka Morocco ameshika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Saleh Huwaij kutoka Libya na Khalid Jasim kutoka Kuwait ambaye ameshika nafasi ya tatu.
Sherehe hizo za kuwaenzi washindi wa mashindano ya kimataifa ya Qur’ani ya Tunisia zimehudhuriwa pia na Mufti wa nchi hiyo Sheikh Othman Battikh, Waziri wa Masuala ya Dini Nuruddin al Khadim na mabalozi wa nchi za Kiislamu na Kiarabu.
Wizara ya Masuala ya Dini ya Tunisia ilikuwa imezialika nchi zote za Kiarabu na Kiislamu kushiriki katika mashindano hayo ambayo yamewakutanisha pamoja makarii na mahafidhi kutoka nchi 19.
Duru ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya Qur’ani ya Tunisia ilifanyika mwaka jana ambapo Amin Puya, karii kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alishika nafasi ya kwanza na hafidhi Zarnushe Farahani pia kutoka Iran alishika nafasi ya pili katika mashindano ya hifdhi ya Qur’ani nzima. 1091903
captcha