IQNA

Agosti 30, Siku ya Kimataifa ya Khitimisha Qur'ani Tukufu

11:21 - August 29, 2025
Habari ID: 3481153
IQNA – Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri kimetangaza kuwa Siku ya Pili ya Kimataifa ya Khatm (Kuhitimisha) Qur'ani Tukufu itaadhimishwa siku ya Jumamosi, tarehe 30 Agosti.

Khatm al-Qurʾan  humaanisha kusoma Qur'an yote kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa kikao kimoja, kama ibada ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuenzi maneno Yake matukufu.

Kwa mujibu wa tovuti ya daralmaref.com, makumi ya maelfu ya washiriki kutoka ndani na nje ya Misri wanatarajiwa kushiriki katika mpango huu wa kiroho ulioanzishwa na Al-Azhar.

Usimamizi wa tukio hili utafanywa na Sheikh Ahmed Al-Tayeb, Imamu Mkuu wa Al-Azhar, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Kiislamu kutoka ndani na nje ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Miongoni mwa washiriki ni ofisi binafsi za kufundisha hifadhi ya Qur'an chini ya usimamizi wa Al-Azhar, Shirika la Kimataifa la Wahitimu wa Al-Azhar, Baraza la Utafiti wa Kiislamu, Chuo Kikuu cha Al-Azhar, pamoja na taasisi nyingine za Kiislamu duniani.

Vilevile, taasisi zilizo chini ya Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar katika nchi mbalimbali kama Indonesia, Nigeria, Uganda, Somalia, Iraq, Afrika Kusini, Chad, Niger, Kenya na Tanzania, zimeonyesha utayari wao wa kushiriki katika mpango huu wenye baraka tele.

Hadi sasa, idadi ya watu waliokwisha jiandikisha kushiriki katika tukio hili kutoka ndani na nje ya Misri imefikia 85,784.

3494393

Kishikizo: qurani tukufu al azhar
captcha