Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Guterres amekemea tangazo la Israel la kukusudia kuliteka Jiji la Gaza, akilitaja kuwa “hatua mpya na hatari ambayo itawalazimisha mamia ya maelfu ya raia waliokwisha kukumbwa na zahma wakimbie tena”.
“Operesheni zilizopanuliwa za kijeshi Gaza City zitakuwa na madhara makubwa,” amesema. “Hili lazima likome.”
Katibu Mkuu ametolea mfano mashambulizi ya kikatili kwenye hospitali, dhidi ya wahudumu wa afya, na wanahabari, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya wiki hii katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis.
“Shambulio moja lilikfuatiwa na jingine likiua raia, wakiwemo wahudumu wa afya na waandishi wa habari waliokuwa wakitekeleza kazi zao muhimu. Yote haya yanafanyika macho ya dunia yanatazama,” amesema, akiongeza kuwa “Lazima kuwe na uwajibikaji.”
Njaa sasa janga lingine la kibinadamu
Guterres amechora taswira ya kutisha ya maisha Gaza, akisema “njaa si tishio linalokuja tena bali ni janga la sasa.”
Ameonya kuwa “Watu wanakufa kwa njaa. Familia zinagawanywa na uhamisho na kukata tamaa. Akina mama wajawazito wanakabiliwa na hatari zisizovumilika. Na mifumo inayodumisha uhai ya chakula, maji, na huduma za afya imebomolewa kwa makusudi”.
“Haya ndiyo mambo halisi ardhini. Na ni matokeo ya maamuzi ya makusudi yanayopinga utu wa msingi.”
Wajibu wa kisheria wa Israel
Katibu Mkuu amesisitiza kwamba kama nguvu inayokalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, Israel lazima iheshimu wajibu wake chini ya sheria za kimataifa.
“Israel lazima ihakikishe upatikanaji wa chakula, maji, dawa na mahitaji mengine muhimu. Lazima ikubali na kuwezesha ufikiaji mkubwa zaidi wa huduma za kibinadamu. Lazima ilinde raia na miundombinu ya kiraia. Na lazima ikomeshe uharibifu wa kile kilicho muhimu kwa maisha ya raia,” amesema Guterres.
Amekumbusha kuhusu hatua za muda za lazima zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki, zinazotaka msaada wa kibinadamu na matibabu usiokuwa na vizuizi kote Gaza “bila kuchelewa na kwa ushirikiano kamili na Umoja wa Mataifa.”
Hakuna visingizio tena, hakuna uongo tena
Licha ya juhudi za Umoja wa Mataifa, Guterres amesema operesheni za kibinadamu zinaendelea “kuzuiwa, kucheleweshwa na kukataliwa” huku wahudumu wa Umoja wa Mataifa wakiendelea kulipa gharama kubwa, ambapo wafanyakazi 366 wameuawa hadi sasa.
“Hili haliwezi kukubalika,” amesisitiza. “Hakuna visingizio tena. Hakuna vizuizi tena. Hakuna uongo tena.”
Mgogoro unaongezeka Ukingo wa Magharibi
Akigeukia Ukingo wa Magharibi, Guterres ameeleza hali kuwa ni ya kutisha sana, akitaja operesheni za kijeshi, ghasia za walowezi, kubomolewa kwa makazi, na upanuzi wa makazi ya walowezi.
“Uidhinishaji wa hivi karibuni wa mpango wa ujenzi wa maelfu ya makazi katika eneo la E1 utatenganisha kimsingi Ukingo wa Magharibi wa kaskazini na kusini na hilo ni tishio kubwa kwa suluhisho la mataifa mawili,” amesema.
“Ninarudia, makazi ya walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki yameanzishwa na yanaendelezwa kinyume na sheria za kimataifa.”
Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena wito wake wa “usitishaji mapigano wa haraka na wa kudumu, ufikiaji wa huduma za kibinadamu usiokuwa na vizuizi kote Gaza, na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote.”
Amehitimisha kwa kusema “Njia ya kuwatesa raia kwa njaa haipaswi kamwe kutumika kama mbinu ya vita. Raia lazima walindwe. Msaada wa kibinadamu lazima upatikane bila kizuizi”.
Utawala wa Kizayuni uliazisha vita vyake vya kikatili dhidi ya Gaza Oktoba 7, 2023. Zaidi ya Wapalestina 63,000, wengi wao wanawake na watoto, wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israeli dhidi ya Gaza.
3494411