IQNA

Makumbusho ya Kiislamu ya Al-Aqsa Yahifadhi Nakala Adimu za Qur'an za Karne Nyingi

11:35 - August 29, 2025
Habari ID: 3481154
IQNA – Makumbusho ya Kiislamu ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa yanahifadhi mkusanyiko wa kipekee wa nakala nadra za kihistoria za Qur'an Tukufu, kuanzia enzi za Umawiyah hadi Uthmaniyah.

Makumbusho haya, yaliyoko ndani ya eneo la Msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu, yanatunza hazina ya takriban nakala 600 za Qur'an Tukufu; kazi adimu zilizotolewa kama zawadi kwa heshima na viongozi wa Kiislamu, masultani, maamiri, wanazuoni, na watu mashuhuri, kuanzia zama za Umawiyah na Abbasiyah hadi Fatimiya, Ayyubiya, Mamluk, na Uthmaniyah.

Nakala hizi zinadhihirisha utofauti mkubwa katika ukubwa, aina ya hati, na mapambo. Miongoni mwa hati zilizotumika ni Kufi, Maghribi, Naskh, Thuluth, na mitindo ya Kiajemi.

Kati ya hazina za kipekee ni Qur'an ya karne ya 8 hadi ya 9 Miladia iliyoandikwa kwa hati ya Kufi, ambayo makumbusho yanaielezea kuwa “Qur'an iliyoandikwa kwa mkono, na maandishi yake yanahusishwa na mjukuu wa nne wa Mtume Muhammad (S.A.W).”

Pia kuna nakala maarufu ya Raba‘ah kutoka Morocco, kazi ya juzuu thelathini iliyoandikwa kwa hati ya Maghribi, iliyotolewa na Sultan Abu al-Hasan al-Marini mwanzoni mwa karne ya 14. Hii ndiyo nakala pekee iliyosalia kati ya tatu zilizotumwa kwa maeneo matakatifu ya Kiislamu: Makka, Madina, na al-Quds.

Makumbusho haya pia yanajivunia Qur'an kubwa zaidi nchini Palestina, iliyoandikwa katika karne ya 14 wakati wa utawala wa Sultan Barsbay wa Mamluk. Nakala hii yenye urefu wa takriban mita moja ni ushahidi wa hazina ya kipekee inayohifadhiwa na makumbusho haya.

 

 

4302136

captcha