Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran, Ayatullah Ahmad Khatami amesema kuwa hotuba iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ufunguzi wa mkutano wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) mjini Tehran imeifedhehesha Marekani, Israel na waitifaki wao.
Ayatullah Khatami amesisitiza kuwa, kufanyika kwa mafanikio mkutano wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) mjini Tehran, kumeonyesha kutengwa utawala za Kizayuni wa Israel na muitifaki wake mkuu Marekani duniani na katika eneo hili la Mashariki ya Kati.
Ayatullah Ahmad Khatami amesema hayo katika khutba za sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran.
Huku akiashiria njama zilizofanywa na utawala wa Kizayuni na Marekani za kuzuia kufanyika mkutano huo wa NAM hapa mjini Tehran, Ayatullah Khatami amesema kuwa, njama zote hizo zilifelishwa kwa ushiriki mkubwa wa wajumbe wa nchi 120 wanachama wa NAM kwenye mkutano huo.
Amesema kwamba, Marekani na Israel zimekasirishwa na mafanikio ya mkutano huo na hasa kwa kuwa umeweza kuwaonyesha walimwengu kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijatengwa kimataifa.
Amezungumzia hutuba iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ufunguzi wa mkutano wa 16 wa NAM uliomalizika Agosti 31 hapa mjini Tehran na kusema kwamba, hotuba hiyo ilikuwa ya kishujaa na iliashiria udharura wa kuwepo uongozi wa kiuadilifu wa masuala ya dunia na kutaka kuitishwe kura huru ya maoni katika ardhi za Palestina itakayowashirikisha Wapalestina wa dini zote wa ndani na nje ya Palestina ili kuamua hatima ya taifa lao. 1093233