Tovuti ya Akhbar-Today imeripoti kuwa, Sheikh wa al Azhar Ahmad Tayyib amepasisha kuasisiwa kituo cha utafiti wa masuala ya Qur’ani kitakachokuwa chini ya Jumuiya ya Kimataifa ya Wahitimu wa Chuo cha al Azhar. Kituo hicho kitakuwa kikijibu maswali yanayoulizwa na watu kuhusu kitabu cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani.
Sheikh Tayyib pia ametilia mkazo udharura wa kuwezeshwa zaidi walimu wa Qur’ani na kutolewa mafunzo zaidi ya sayansi ya Qur’ani kwa walimu hao.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Masuala ya Idara la Jumuiya ya Kimataifa ya Wahitimu wa al Azhar Usama Yasin amesema kuwa kuasisiwa kituo cha utafiti wa masuala ya Qur’ani kunafanyika kwa lengo la kuimarisha kiwango cha kielimu na kiutamaduni cha wanafunzi wa al Azhar na kuwatayarisha kwa ajili ya kuelewa vyema kitabu hicho cha mbinguni.
Usama Yasin ameongeza kuwa mbinu inayotumika ni ile ya kujua aya za nasikh na mansukh, asbabu nuzul, mlingano na uwiano baina ya aya tofauti za Qur’ani na muujiza za Qur’ani Tukufu
Amesema kituo hicho pia kitachunguza maisha ya makarii wa Qur’ani, jinsi kiraa mbalimbali za Qur’ani zilivyotokea, majibu na maswali yanayotolewa kuhusu suala hilo na kadhalika. 1096132