Viongozi wa Libya wamethibitisha tukio hilo na kusisitiza kuwa, mbali na balozi huyo kuuawa, wanadiplomasia watatu wa ubalozi huo wa Marekani pia wameuawa. Jana jioni maelfu ya Walibya waliuvamia ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi wakilaani hatua ya Marekani kuruhusu kusambazwa kwa filamu iliyomvunjia heshima mtukufu Mtume Muhammad (saw). Aidha waandamanaji waliokuwa wamejawa na hasira walifyatua risasi angani kabla ya kuingia ndani ya ubalozi huo na kuuchoma kwa moto.
Hivi karibuni Muisrael mmoja aishie Marekani alisambaza filamu inayomvunjia heshima Mtume wa Uislamu Muhammad (saw) hatua iliyozusha hasira kali kwa Waislamu kote duniani. Filamu hiyo iliyopewa jina la "Innocence of Muslims" imetengenezwa na Sam Bacile ambaye ni Muisrael Mmarekani mwenye umri wa miaka 54. Muisrael huyo ameutusi Uislamu kuwa ni ugonjwa wa saratani. Bacile anasema filamu hiyo imetengenezwa kwa ufadhili wa dola milioni tano zilizotolewa na Mayahudi 100.
Filamu hiyo pia imeungwa mkono na Kasisi Terry Jones wa kanisa la Dove World Outreach Center katika mji mdogo wa Gainsville katika jimbo la Florida nchini Marekani. 1097124