Rais Barack Obama wa Marekani amesema kuwa filamu iliyoutusi Uislamu ambayo imezusha hasira na malalamiko makubwa ya Waislamu kote duniani inaivunjia heshima pia Marekani lakini wakati huo huo amedai kuwa, serikali ya Washington haiwezi kuzuia usambazaji na kuonyeshwa kwake!
Bila ya kuashiria hata kidogo kwamba uhuru wa kusema na kujieleza una mipaka, Rais Barack Obama asema katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, katiba ya Marekani inalinda uhuru wa kusema na kujieleza na kwa sababu hiyo serikali yake haiwezi kuzuia filamu kama hiyo inayomvunjia heshima Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Barack Obama amefumbia macho nafasi adhimu ya Mtume Muhammad (saw) na ukweli kwamba kumvunjia heshima mtukufu huyo ni kudharau matukufu ya Waislamu zaidi ya bilioni moja na nusu.
Ametetea hatua ya serikali ya Marekani ya kutozuia utengenezaji na kuonyeshwa filamu hiyo kwa kujilinganisha yeye na matukufu ya Kiislamu akisema: Mimi ni Rais wa jamhuri na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Marekani lakini nakubali kusikia maneno machafu yanayotolewa kila siku na wananchi dhidi yangu na ninalinda haki yao hiyo (ya kutusi). 1107503