IQNA

Viongozi wa kidini wa Ufaransa walaani kuendelea kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu

21:25 - October 06, 2012
Habari ID: 2426449
Viongozi wa Kiislamu, Kiyahudi, Kibuda na Kikristo kaskazini mwa Ufaransa wamelaani vikali vitendo vya kuendelea kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa tovuti ya nordeclair, viongozi hao walitoa taarifa siku ya Ijumaa wakilaani vikali utengenezaji na usambazaji wa filamu pamoja na vikatuni vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (asw) nchini Marekani na Ufaransa.
Wamelaani pia hujuma dhidi ya misikiti katika nchi za Magharibi na hasa nchini Ufaransa na kusema kwamba jambo hilo linakwenda kinyume na thamani za kidini.
Viongozi hao wa kidini wamesema wanapinga hatua na jambo lolote linalozusha fitina na mifarakano baina ya wafuasi wa dini tofauti na kuwataka wafuasi hao kujiepusha na vitendo vyovyote vya ulipizaji kisasi na vinavyokwenda kinyume na misingi ya sheria.
Wamesema kutengenezwa filamu hiyo ya dharau dhidi ya matukufu ya Kiislamu katika kipindi hiki cha kukaribia kufanyika uchaguzi huko Marekani ni ishara ya wazi kuwa kuna baadhi ya watu wanaotaka kutumia vibaya hali hiyo kwa lengo la kuzusha uchochezi wa kidini katika jamii ya nchi hiyo. Wamewataka wananchi wote wa Ufaransa kuzingatia umoja na mshikamano bila kujali rangi wala itikadi zao za kidini. 1113904
captcha