IQNA

Harakati ya Ukombozi wa al Aqsa yamtaka Mursi aombe radhi

21:56 - October 22, 2012
Habari ID: 2436206
Harakati ya Ukombozi wa al Aqsa ya Misri imelaani barua ya upendo na urafiki iliyoandikwa na Rais wa nchi hiyo Muhammad Mursi kwa Rais wa utawala ghasibu wa Israel Shimon Perez na imemtaka Mursi aliombe radhi taifa la Misri kutokana na barua hiyo iliyojeruhi hisia za Wamisri.
Gazeti la al Mash’had limeripoti kuwa, Harakati ya Ukombozi wa al Aqsa imetangaza kuwa kamwe haitaitambua rasmi Israel kama nchi na haikubaliani na sentensi zilizoakisi upendo na urafiki za barua ya Mursi kwa Shimon Perez.
Msemaji wa Harakati ya Ukombozi wa al Aqsa Mahmoud Gharib amepinga sababu zilizotolewa na msemaji wa Rais wa Misri akihalalisha barua hiyo na kusema si sahihi kwa rais wa kwanza aliyechaguliwa na wananchi wa Misri baada ya mapinduzi ya wananchi ya tarehe 25 Januari kuzungumza kwa kutumia maneno ya upendo na urafiki kama hayo na Shimon Perez ambaye ni adui wa umma na muuaji wa Waislamu.
Gharib amemtaka Rais Muhammad Mursi wa Misri aliombe radhi taifa kutokana na barua hiyo.
Tarehe 17 Oktoba Rais Muhammad Mursi wa Misri alimteuwa Atif Muhammad Salim kuwa balozi mpya wa nchi hiyo katika utawala wa Kizayuni wa Israel na kumkabidhi barua ya Shimon Perez Rais wa utawala haramu wa Israel ambayo ilikuwa na maneno yanayoakisi upendo na urafiki akiutakia mafanikio na ustawi utawala huo ghasibu. 1123346
captcha