Hamas imeeleza matarajio kuwa katika kipindi cha pili cha uongozi wake Rais Barack Obama wa Marekani ataheshimu haki za Wapalestina na kuacha kuupendelea utawala ghasibu wa Israel.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri imesema kuwa, Hamas inamtaka Obama kutazama upya siasa za nje za Marekani zinazohusiana na masuala ya Palestina na nchi za Kiarabu na kukomesha mwenendo wa kuipendelea Israel.
Taha Nunu ambaye pia ni msemaji wa Hamas amesema inatarajiwa kuwa Obama ataheshimu haki za Wapalestina na kusitisha siasa za kindumakuwili na kuupendelea utawala ghasibu wa Israel.
Amesema miaka minne iliyopita baada ya Barack Obama kushinda uchaguzi wa Rais alisikika akisema maneno mazuri kuhusu Mashariki ya Kati na kadhia ya Palestina lakini utendaji na siasa zake zilikwenda kinyume kabisa na matamshi yake.
Barack Obama alichaguliwa tena jana kuongoza Marekani kwa kipindi kingine cha miaka minne. 1133483