IQNA

Siku Kuu ya kitaifa yatangazwa Ukanda wa Ghaza

11:42 - November 23, 2012
Habari ID: 2453160
Harakati ya muqawama ya wananchi wa Palestina Hamas ilitangaza jana Alhamisi kuwa sikukuu ya kitaifa kutokana na ushindi walioupata hivi karibuni wananchi wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza dhidi ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Msemaji wa Hamas aliwataka Wapalestina wote kusherehekea sikukuu hiyo na kwenda kuzitembelea familia za mashahidi na majeruhi wa vita. Ismail Haniya Waziri Mkuu wa serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Palestina ameeleza kufurahishwa kwake na makubaliano ya usitishaji vita yaliyofanyika kutokana na upatanishi wa Misri na kusisitiza kuwa, binafsi anajifakharisha na msimamo ulioonyeshwa na wananchi wa Ghaza katika kukabiliana na jinai za Wazayuni. Amesema kuwa, kusimama kidete muqawama wa Wapalestina mbele ya mashambulizi ya mizinga, makombora na mabomu ya majeshi ya Israel kwa muda wa siku nane, kumewafanya Wazayuni waangalie upya uendelezaji wa jinai zao huko Ghaza. Mapigano hayo yaliyodumu kwa siku nane, yalipelekea Wapalestina wasiopungua 160 kuuawa shahidi na wengine 1,200 kujeruhiwa, idadi ambayo haiwezi kulinganishwa na ile ya mashahidi na majeruhi wanawake na watoto katika vita vya siku 22 vya mwaka 2008. Ulimwengu umepokea kwa mtazamo chanya usitishaji mapigano hayo. Hardeep Singh Puri Mwakilishi wa India katika Umoja wa Mataifa na ambaye pia ni Mwenyekiti wa mzunguko wa Baraza la Usalama la umoja huo, ameelezea kufurahishwa kwake na hatua hiyo na kuwashukuru Rais wa Misri na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutokana na idili na juhudi zao za kutatua mgogoro huo.

Hivi sasa wananchi wa Ghaza wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, mafuta na madawa. Wakati wanamuqawama wa Kipalestina walipokuwa wakikabiliana na majeshi ya Wazayuni kwenye vita hivyo visivyokuwa na mlingano, walitoa funzo kwa utawala wa Tel Aviv, funzo ambalo lilivuruga mahesabu ya watawala wa utawala huo na kuwafanya wapate kipigo wasichokitarajia. Kushambuliwa kwa makombora na roketi za wapiganaji wa Hamas huko Tel Aviv na miji mingine ya utawala wa Israel, ni ujumbe tosha kwa Wazayuni kwamba wasithubutu tena kuliangalia eneo la Ghaza kama uwanja wa kufanyia majaribio ya silaha zao za kijeshi.

Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Israel ameuongoza utawala muflisi zaidi wa Israel katika kipindi cha miongo ya hivi karibuni, kwani alikuwa ameanzisha vita vya Gaza kwa malengo yake ya kisiasa. Hii ni katika hali ambayo, hatua ya kukubali kufanyika mapatano ya kusitisha mapigano ni aina ya kukiri kushindwa kwenye vita hivyo, ambapo hivi sasa vyama vya upinzani vinamsakama na kustafidi kisiasa na fedheha hiyo ya Netanyahu. Shaul Mofaz kiongozi wa chama cha Kadima, mara baada ya kutangazwa usitishaji mapigano alisikika akinena kwamba, Hamas ndio mshindi kwenye vita hivyo na Israel mshindwa, matamshi ambayo bila shaka yatamvurugia Netanyahu fursa ya ushindi kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa Januari mwaka 2013. Bila shaka ulimwengu umeshuhudia jinsi utawala wa Kizayuni wa Israel ulivyoshindwa katika vita vya hivi karibuni vya siku nane huko Ghaza. Hii ni katika hali ambayo walimwengu bado hawajasahau kumbukumbu ya kushindwa kwingine kwa fedheha utawala huo ghasibu katika vita vya siku 22 vya mwaka 2008.
1142522
captcha