Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi wakati akitoa darsa ya fiqhi ambapo amewashukuru mno wananchi wa Iran kutokana na tabasuri na muono wao wa mbali, ushujaa na kuzielewa vizuri alama za nyakati na hivyo kuunda hamasa adhimu ya wananchi katika maadhimisho ya Bahman 22 (Jumapili Februari 10, 2013, zilipofikia kileleni sherehe za miaka 34 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran). Aidha amekutaja kujitokeza kwa wingi na kwa sifa za namna hiyo wananchi wa Iran katika maadhimisho hayo kuwa ni tukio kubwa sana na kusisitiza kwamba: Kushiriki kwenye sherehe hizo watu wa matabaka yote, kuanzia wazee hadi vijana, wake kwa waume tena katika mazingira ambayo miaka 34 imepita tangu kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu ambayo inabidi tumshukuru Mwenyezi Mungu katika umri wetu wote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelinganisha baina ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yanayofanyika nchini Iran na yale yanayofanyika kuadhimisha mapinduzi mengineyo duniani na kuongeza kuwa: Kitu bora kabisa kinachoyapambanua Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengineyo duniani ni kuwa, mapinduzi haya ya Iran ni ya wananchi wenyewe; na wenyewe wananchi wanalitambua hilo na kazi ya kufanya sherehe za maadhimisho ya mapinduzi hayo inafanywa na wananchi wenyewe. Ni kwa sababu hiyo ndio maana wananchi wa Iran wanaulinda kwa kila hali utajiri wao huo ambao ndio uliowaletea heshima na uhuru na wakati wowote wanapopata fursa, wananchi hao hujitokeza kwenye medani kuwaonesha walimwengu uungaji mkono wao kwa Mapinduzi yao ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amemshukuru kila mwananchi wa Iran kutokana na kujitokeza kwenye medani katika wakati mwafaka na kuongeza kuwa: Wananchi wa Iran wamejitokeza vilivyo na kwa hamasa kubwa kutangaza uungaji mkono wao wa kila upande kwa Jamhuri ya Kiislamu na Mapinduzi ya Kiislamu katika ule wakati hasa ambao adui alitaka awaone wananchi hao wanajiweka mbali na Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Amesema, kwa kujitokeza kwao huko kwa wingi na kwa shauku na hamasa kubwa, wananchi wa Iran wamefelisha njama za maadui na kuwakatisha tamaa kabisa.
Vile vile amesisitiza kuwa, katika propaganda zao, maadui wanafanya njama za kuonyesha kuwa nuru ya medani hiyo adhimu ya wananchi imefifia na wakati huo huo ameongeza kuwa: Tab'an maadui hao wanauona uhakika wa mambo katika medani na wanajua vyema ukweli wa mambo na ndio maana mwisho wa yote wanakiri kuwa haiwezekani kukabiliana na taifa lenye sifa kama hizi.
1186615