Kituo cha On Islam kimeripoti kuwa, kituo cha simu cha kutoa msaada kwa Waislamu wa Uingereza kilichoanzishwa mwaka jana baada ya mwaka mmoja kimetoa ripoti kuhusu ubaguzi na ukatili unaofanywa dhidi ya Waislamu nchini humo.
Ripoti ya kituo hicho imeikosoa polisi ya Uingereza kwa kuzembea na kutowapa msaada wahanga Waislamu.
Mratibu wa laini ya simu iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu maarufu kwa jina la "Tell Mama" amesema kuwa, kituo hicho kinafanya jitihada za kuwasiliana na polisi na wanasiasa wa Uingereza ili wachukue hatua za kuondoa hofu na chuki zinazowalenga Waislamu nchini humo.
Fayyadh Magul amesema, wanawake na hata wanaume Waislamu wamekuwa wakilengwa kwa mashambulizi ya chuki, ubaguzi, na ukatili kupitia mitandao ya intaneti, maeneo yao ya kazi, mitaani na hata maeneo ya ibada.
Ameongeza kuwa ripoti iliyokusanywa na kituo hicho ni ya mwaka mmoja uliopita na inaonesha kuwa wanawake Waislamu ndio wahanga wakuu wa mashambulizi hayo ya kibaguzi.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa silimia 58 ya kesi 630 za mashambulizi ya kibaguzi zilizoripotiwa dhidi ya Waislamu katika kipindi hicho iliwahusu wanawake.
Ripoti hiyo pia imeonesha kuwa wanawake Waislamu wanaovaa vazi la hijabu ndio wanaolengwa zaidi kwa kupigwa mitaani. 1202581