IQNA

Ahmadinejad:Taifa la Iran litaendela kuvunja njama za maadui

22:19 - March 20, 2013
Habari ID: 2513119
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ujumbe wa Nowruz kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1392 Hijria Shamsiya na kusisitiza kuwa taifa la Iran litaendelea na harakati ya kuvunja kikamilifu njama za maadui. Ameongeza kuwa taifa la Iran liteendelea na njia yake ya ustawi katika nyanja zote ili kufikia uadilifu wa kimataifa.
Katika ujumbe wake, Rais Ahmadinejad ametoa salamu za kheri na fanaka kwa Wairani wote na kila ambaye anasherehekea Nowruz. Rais Ahmadinejad ameendelea kusema kuwa taifa la Iran limeshika kasi katika ustawi wa nyanja mbali mbali za kisayansi, kiviwanda, kilimo, kiteknolojia, kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi na kimichezo. Amesema ustawi huu unazidi kuimarika siku hadi siku. Rais Ahmadinejad amesema kuwa, mwaka mpya wa Kiirani wa 1392 utakuwa mwaka uliojaa izza na baraka na kwamba hakuna shaka kuwa taifa la Iran litaibuka mshindi. Kuhusiana na uchaguzi ujao wa rais wa Iran utakaoofanyika mwezi Juni, Ahmadinejad amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuwepo uchaguzi wenye msisimuko na utakaoshirikisha idadi kubwa ya wananchi.

Sherehe za Nowruz zimeanza leo kote Iran ambapo wananchi wengi wameadhimishwa kuingia mwaka mpya kwa kujitokeza katika maeneo ya ibada hasa katika Haram Takatifu ya Imam Ridha AS. Aidha sherehe za Nowruz zimefanyika pia katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita.

Kati ya nchi ambazo Nowruz husherehekea ni kama vile Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kirghizstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi Machi 21 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira. Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, siku kuu ya Nowruz hueneza thamani za amani na mshikamano wa vizazi katika familia sambamba na kuleta maelewano na ujirani mwema na hivyo kuwa na mchango mkubwa wa urafiki baina ya watu wa jamii mbali mbali.

Inafaa kuashiria hapa kuwa katika ustaarabu wa Kiswahili, Nowruz huadhimishwa japo katika mwezi tofauti na ule wa mwanzo wa machipuo hapa Iran. Sherehe hizi hasa zinashuhudiwa Zanzibar ambapo Nowruz hujulikana kama Nairuzi yaani siku ya mwaka au mwaka kogwa.
1206373
captcha