IQNA

Imam Khamenei: Iwapo Israel itaishambulia Iran, Tel Aviv itasawazishwa na udongo

11:49 - March 23, 2013
Habari ID: 2513231
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria matamshi yanayotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kushambulia taasisi za nyuklia za Iran na kusema kuwa, Israel inajua na kama haijui inapaswa kutambua kwamba, iwapo itajaribu kufanya hivyo makombora ya Iran yataisawazisha na udongo miji ya Tel Aviv na Haifa.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Alkhamisi jioni kwa mnasaba wa siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Kiirani wa 1392 Hijria Shamsia. Alitoa hotuba muhimu sana mbele ya umati mkubwa wa maelfu ya wafanyaziara na watu wanaoishi jirani na Haram toharifu ya Imam Ali bin Musa Ridha AS waliokuwa wamekusanyika kwenye haram hiyo.
Sambamba na kutoa tathimini ya mafanikio na maendeleo ya kimsingi na makubwa liliyopata taifa la Iran katika mwaka uliopita wa 1391 Hijria Shamsia licha ya kuweko vizuizi vingi na vikubwa sana vya kivitendo na kipropaganda vya watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran, ametolea ufafanuzi nukta kadhaa za kimsingi kuhusu mazungumzo na Marekani na pia masuala ya lazima na yanayohitajika katika hamasa ya kiuchumi na hususan wajibu wa kuacha kutegemea mafuta katika bajeti ya nchi na kuzipa mazingatio makubwa siasa kuu za kiuchumi pamoja na kuchukua hatua za kiwerevu kabla adui hajatekeleza njama zake.
Vile vile amezungumzia mambo ya lazima katika hamasa ya kisiasa na hasa hasa kushiriki vilivyo wananchi katika uchaguzi wa mwaka huu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, katika uchaguzi huo inabidi watu wa mitazamo na mawazo tofauti na wa mirengo mbali mbali ambao ni wafuasi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, washiriki kwenye uchaguzi huo na kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na hima ya wananchi wa Iran kuweze kushuhudiwa uchaguzi wa kufana kwani uchaguzi wa Rais una athari kubwa katika masuala yote makuu ya nchi.
Ayatullah Udhma Sayyid Khamenei ameanza hotuba yake kwa kutoa mkono wa baraka kwa mara nyingine tena kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia na baadaye ametoa tathmini juu ya nukta chanya na nukta dhaifu zilizoshuhudiwa nchini Iran katika mwaka uliopita na kusisitiza kuwa ni jambo la dharura kuwa na mipangilio mizuri kwa kutegemea msingi wa tathmini hiyo kuu. Ameongeza kuwa: Kama ambavyo mtu anahitajika mara zote kutathmini na kuchunguza masuala yake ya kila siku, ni vivyo hivyo katika masuala ya nchi, kunahitajika tathmini na ukadirifu wa kitafa na hilo ni jambo muhimu sana kwani linatoa ibra na funzo na kuonesha njia ya kufuata katika masuala yaliyopo na yanayokuja.
Vile vile ameashiria jinsi mataifa, wasomi na watu muhimu wa nchi mbali mbali wanavyoangalia kwa kina kazi na mafanikio ya taifa la Iran ili waweze kupata somo na kigezo cha kufuata, na namna maadui wanavyoangalia kwa kina mafanikio ya taifa la Iran na baadhi ya wakati udhaifu unaojitokeza kwa taifa hilo na kusisitiza kwamba: Katika upande huo pia taifa la Iran linapaswa kuwa na mtazamo mkuu na unaokubaliana na uhakika wa mambo na vile vile liwe na tathmini sahihi kuhusu hali ilivyo nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kuratili na kutathmini hali ilivyo nchini kwa kuangalia tu masuala kama vile ughali wa maisha, kupungua uzalishaji katika baadhi ya sekta za uzalishaji na mashinikizo ya kiuchumi, ni kupima mambo nusu nusu, si ukadirifu kamili na wala si tathmini iliyosimama juu ya uhalisia wa mambo.
Amesisitiza kuwa: Kipimo na tathmini sahihi ni kwamba, pamoja na kuweko udhaifu na matatizo katika medani hiyo adhimu iliyojaa changamoto kwa taifa la Iran, yalikuweko pia maendeleo na mafanikio makubwa na kwa kuzingatia uhakika huo tutaona kuwa, taifa la Iran limepata mafanikio makubwa na limedhihiri kifua mbele na kwa ushujaa katika medani hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna Marekani inavyotoa tathmini yake waziwazi kuhusiana na kuliwekea vikwazo na mashinikizo taifa la Iran kwa kusema bila kificho kuwa vikwazo hivyo vimewekwa ili kulifanya kilema taifa la Iran na kuongeza kuwa: Katika medani hiyo iliyojaa changamoto, taifa la Iran kwa werevu wa hali ya juu na kwa nguvu zake nyingi, limefanikiwa kubadilisha vitisho hiyo kuwa fursa nzuri kwake na mfano wake ni kama mtu anayechukua ubingwa katika michezo, ambaye huibuka na ushindi baada ya kuvuuka kwenye mapambano na ushindani mkubwa ulioambatana na tabu na mashaki mengi na juhudi zisizochoka na hatimaye kupongezwa na watu wote kwa ushindi anaoupata.
Ameongeza kuwa: Iwapo kipimo na tathmini ya masuala ya nchi na mazingira yake itakuwa kwa namna hiyo, bila ya shaka yoyote tutaona kuwa, bingwa wa medani hiyo adhimu ni taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mafanikio na ufanisi wa taifa la Iran katika medani hiyo iliyojaa changamoto ni mkubwa kiasi kwamba ufanisi huo hata umesifiwa na weledi wa mambo wanaoangalia mambo kwa kina na wasomi na watu muhimu na wenye ushawishi wa kisiasa katika nchi mbali mbali duniani na hata katika nchi zinazoitakia mabaya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameliashiria lile kundi la watu ambao daima hawafurahishwi na maendeleo ya Iran na kusisitiza kuwa, kundi hilo ambalo linaundwa na maadui wa taifa la Iran linatumia mbinu namna mbili kukabiliana na maendeleo ya Iran: 1 - Kuweka vizuizi vya kivitendo kama vile vikwazo, vitisho na kuwashughulisha viongozi, wasomi na wananchi wa Iran na masuala ya pembeni yasiyo na kipaumbele chochote, na 2 - Kufanya propaganda kubwa sana za kuficha maendeleo ya taifa la Iran ili walimwengu wasiyaone maendeleo hayo na kukuza kupindukia udhaifu unaojitokeza kwa taifa hili (ili walimwengu wahisi hakuna maendeleo yoyote ambayo taifa la Iran limeyapata).
Amesema, katika upande huo, mwaka wa 1391 Hijria Shamsia ulikuwa ni mwaka wa kazi nyingi kwa watu wasiolitakia mema taifa la Iran ikilinganishwa na miaka ya kabla yake na kuongeza kuwa: Maadui wa taifa la Iran wamesema wazi kuwa, lengo lao ni kulifanya kilema na kulipigisha magoti taifa la Iran, hivyo iwapo taifa la Iran litakabiliana vilivyo na vikwazo vyote hivyo na kuendelea kuwa imara bila ya kutetereka bali na kuzidi kupata maendeleo katika nyuga tofauti, jambo hilo kwa hakika litawaaibisha maadui hao.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza maswali mawili: 1 - Liko wapi pango kuu la njama dhidi ya taifa la Iran? 2 - Maadui wa taifa la Iran ni akina nani?
Akijibu swali la kwanza, Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Kituo kikuu cha njama dhidi ya taifa la Iran ni Marekani kiasi kwamba leo hii na baada ya kupita miaka 34 ya njama dhidi ya taifa la Iran, unapotaja neno adui tu, akili za wananchi wa Iran moja kwa moja zinalenga kwa Marekani.
Ameongeza kuwa: Viongozi wa Marekani wanapaswa kutaamali na kulizingatia kwa kina suala hilo na wajiulize, kwa nini akili ya taifa la Iran kuhusu adui wakati wote inalenga moja kwa moja kwa Marekani?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema kuhusu maadui wa taifa la Iran kwamba: Mbali na Marekani ambaye ni adui nambari moja na ni kituo kikuu cha njama dhidi ya Iran, kuna na maadui wengineo ambapo serikali khabithi ya Uingereza ni miongoni mwa maadui hao, lakini Uingereza yenyewe haina uhuru, bali inafuata mkumbo, ni mkamilishaji tu wa njama za Marekani.
Aidha katika sehemu hiyo ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameitahadharisha serikali ya Ufaransa na kusema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuwa na tatizo na serikali na wala taifa la Ufaransa, lakini serikali ya Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni na hasa hasa wakati wa utawala wa Sarkozy imekuwa ikifuata siasa za uadui wa wazi wazi dhidi ya taifa la Iran. Lakini serikali ya Ufaransa inapaswa kujua kuwa, siasa hizo ni ghalati na ni kosa kubwa kuendelea nazo, si siasa za kimantiki, bali watu wenye busara na akili, hawamfanyi mtu ambaye si adui yao kuwa adui yao.
Vile vile ameuashiria utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa: Utawala ghasibu wa Kizayuni hata hauko katika daraja na hadhi ya kuwa adui wa taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia baadhi ya vitisho vinavyotolewa na viongozi wa utawala wa Kizayuni vya kudai kuwa vitaishambulia kijeshi Iran na kusisitiza kwamba: Kama (Wazayuni) watathubutu kufanya ghalati na kosa lolote lile (la kuishambulia Iran), basi Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran itaifutilia mbali miji ya Tel Aviv na Haifa na kuisawazisha na ardhi mara moja.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Daima utawasikia Wamarekani wanawatumia maadui hao wachache wa taifa la Iran na kuwapa jina lisilo sahihi. Wanaziita nchi hizo "Jamii ya Kimataifa" wakati ambapo "Jamii ya Kimataifa" kamwe haina uadui na Muirani na wala Iran ya Kiislamu.
Baada ya kuwatangaza maadui wa kweli na wachache wa Iran, Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kutoa ufafanuzi kuhusu hatua za kiadui zilizochukuliwa na maadui hao mwaka uliomalizika wa 1391 Hijria Shamsia na kuongeza kuwa: Tofauti na madai yao ya kujifanya ni marafiki wa taifa la Iran, Wamarekani tangu mwanzoni kabisa mwa mwaka uliopita ilishadidisha vikwazo vyake na kuiwekea Iran vikwazo vikubwa vya mafuta na Benki na hadi hivi sasa wanashikilia kuwa si maadui wa taifa la Iran licha ya kuchukua kwao hatua hizo za kiuadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, siasa hizo ni kuendelea na siasa zile zile za "kuficha makucha ndani ya glovu za mahameli" (siasa za kuuma na kupuliza) na kuongeza kuwa: Tofauti kabisa na madai yao ya kudanganya watu, Wamarekani walianzisha mpango maalumu uliokuwa umepangiliwa vyema dhidi ya taifa la Iran na walitaraji kuwa baada ya kupita miezi michache tu, taifa la Iran litasalimu amri na kupigia magoti siasa zao za kibeberu na litaachana na harakati zake za kujiletea maendeleo ya kielimu, lakini kilichojiri kilikuwa ni kitu tofauti kabisa na matarajio ya watu hao wasiolitakia mema taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia jinsi viongozi wa Marekani walivyoshindwa kuficha furaha zao kutokana na taathira za vikwazo vyao na matamshi ya baadhi ya viongozi wa Iran kuhusu suala hilo na kuongeza kuwa: Ni kweli vikwazo hivyo vimetuathiri, lakini havikuwa na taathira iliyokusudiwa na maadui hao.
Ameongeza kuwa: Kama vikwazo vimeacha athari sababu yake kuu ni kuwa uchumi wa nchi unategemea mafuta na ni kwa sababu hiyo ndio maana likawa ni jambo la wajibu kuwa na uchumi usiotegemea mafuta na hilo ndilo linalopaswa kuwa suala la kupewa kipaumbele kikuu katika mipango ya serikali ijayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia matamshi yake aliyoyatoa miaka kadhaa nyuma kuhusu wajibu wa kufikia katika hatua ambayo itawezekana kufunga visima vya mafuta na kuendesha nchi bila ya kutegemea hata tone moja la mafuta na kuongeza kuwa: Wakati huo baadhi ya watu ambao wenyewe wanajiita wasomi walitoa tabasamu za kejeli kuhusiana na matamshi hayo na wakasema; hivi kitu kama hicho kinawezekana kweli?
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Ni jambo linalowezekana kabisa kufikia kwenye uchumi usiotegemea mafuta hata kidogo, lakini jambo hilo lina masharti yake nayo ni kuwa na mipangilio sahihi.
Baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu hatua za chuki zilizochukuliwa na maadui katika mwaka uliopita wa 1391 Hijria Shamsia dhidi ya taifa la Iran katika upande wa kiuchumi, ameashiria njama za maadui hao katika upande wa kisiasa na kusema kuwa: Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran katika upande wa kisiasa, ni kujaribu kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itengwe kimataifa, lakini kufanyika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM mjini Tehran na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wakuu na viongozi wa ngazi za juu wa nchi wanachama wa harakati hiyo na kuipongeza Iran kutokana na maendeleo yake ya kustaajabisha ya kisayansi na kiteknolojia, kulifelisha kikamilifu njama hizo za maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hatua nyingine iliyochukuliwa na maadui katika mwaka uliopita ni kujaribu kuwatia wasiwasi wananchi wa Iran na kuwafanya wajiweke mbali na mfumo wao wa utawala yaani Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Kushiriki kwa wingi mno na kwa hamasa na shauku kubwa wananchi wa Iran katika maandamano ya Bahman 22 (wakati wa maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu) na kuonyesha mapenzi yao makubwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu, kulitoa pigo jingine kubwa kwa maadui.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja baadhi ya njama zilizoshindwa katika masuala ya usalama na njama za kutaka kupunguza ushawishi na nguzu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili kuwa ni hatua nyingine za kiadui zilizochukuliwa na watu wasiolipendea mema taifa la Iran katika mwaka uliopita wa Hijria Shamsia.
Ameongeza kuwa: Uwepo wa Iran yenye nguvu nyuma ya vita vya siku nane vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina na kwa mara ya kwanza kuweza wanamapambano wa Palestina kuupigisha magoti utawala wa Kizayuni na vile vile kukiri maadui wa Iran kuwa masuala ya Mashariki ya Kati hayawezi kutatuliwa bila ya kushirikishwa Iran ni ushahidi mwingine unaothibitisha kufeli njama za maadui katika upande huo.
Vile vile amesisitiza kuwa: Mashinikio yote haya na uadui wote huu hususan vikwazo vya kila nui pamoja na kwamba vimekuwa na taathira hasi, lakini pia vimekuwa na athari kubwa chanya kwa taifa la Iran na muhimu kuliko yote ni kuwa vikwazo na mashinikizo hayo yamepelekea kupata nguvu uwezo ya ndani ya Iran na vipaji vya wananchi wa taifa hili kulikopelekea kufanikishwa kazi kubwa muhimu na za kimsingi katika mwaka uliopita.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia baadhi ya maendeleo na mafanikio makubwa na ya kimsingi liliyopata taifa la Iran mwaka 1391 Hijria Shamsia licha ya kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya maadui na kuongeza kuwa: Kupatikana vyanzo vingine vipya vya mafuta na vyanzo vingine vipya vya urani, kuanzisha na kupanua vinu na viwanda vya mafuta, kuchukuliwa hatua za kimsingi katika upande wa barabara na katika masuala ya nishati, kupatikana mafanikio makubwa ya kisayansi na kiteknolojia ikiwa ni pamoja na kutuma anga za juu satalaiti ya Nahid na satalaiti ya utafiti yenye kiumbe hai, kutengeneza ndege za kisasa kabisa za kivita, kuzalisha dawa muhimu mno zenye michanganyiko tofauti mipya na kushika nafasi za kwanza na daraja za juu katika masuala ya kielimu, kuongezeka kasi ya maendeleo ya kielimu, kuongezeka idadi ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu na wasomi wa Kiirani yote hayo ni maendeleo, ufanisi na mafanikio makubwa liliyopata taifa la Iran katika mwaka ambao maadui walikusudia kulifanya kilema taifa la Iran kupitia vikwazo vyao hivyo.
Amesisitiza kuwa: Somo kubwa linalopakatikana kutokana na ufanisi na mafanikio hayo makubwa ya mwaka uliopita wa 91 ni kwamba taifa lililo hai kamwe haliwezi kupigishwa magoti na vikwazo, mashinikizo na mibinyo ya adui.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha pia nukta dhaifu zilizoshuhudiwa katika uchumi wa Iran kwenye mwaka uliopita na kuongeza kuwa: Kitendo cha uchumi wa nchi kutegemea mafuta, kutozingatiwa siasa kuu za kiuchumi, kukumbwa na siasa zile zile za kila siku ni miongoni mwa nukta hasi ambazo viongozi nchini na hasa serikali ijayo inapaswa kuyazingatia na kuyapa uzito wa hali ya juu na ijulikane kwamba nchi hivi sasa inahitajia kuwa na siasa kuu za kiuchumi, zilizo wazi, zilizopangiliwa vizuri na zenye umakini wa hali ya juu.
Pia amesema, somo jingine linalopatikana kutoka katika mwaka ulioisha wa 1391 Hijria Shamsia ni kujulikana uwezo mkubwa ilio nao Iran na kuongeza kuwa: Kadiri uwezo wa nchi unavyokuwa mkubwa na viongozi wa nchi wanapokuwa na umoja na mshikamano na kufanya kazi zao kwa umakini na tadibiri ya hali ya juu, ndivyo taathira hasi za vitendo vya kiuadui vya adui zinavyozidi kuwa ndogo sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kwamba, mbali na masuala ya uchumi, masuala yanayohusiana na amani, usalama wa wananchi, maendeleo ya kielimu, uhuru na heshima ya taifa, nayo ni muhimu kwa nchi na kuongeza kuwa: Taifa la Iran kutokana na mafanikio liliyopata mwaka uliopita limeweza kuwathibitishia walimwengu kuwa, kutokuwa kibaraka wa Marekani na madola makubwa ya kibeberu si tu hakulifanyi taifa kubaki nyuma kimaendeleo, bali kunalifanya taifa hilo liwe huru na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Baada ya kutoa tathmini jumla kuhusu hali ilivyokuwa katika mwaka ulioisha wa 91, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia nukta mbili kuhusu mustakbali au mambo ambayo yanaweza kuwa funzo kutoka katika masuala ya mwaka uliopita.
Kuelewa njama za adui kabla ya kutekeleza njama zake hizo na kupambana kibusara na kwa umahiri wa hali ya juu na njama za maadui, ilikuwa ni nukta ya kwanza iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu hiyo ya hotuba yake.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Hatua ya wasomi vijana wa Kiirani ya kulidhaminia taifa fueli kutoka katika urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 kwa ajili ya kinu cha utafiti wa nyuklia cha Tehran na kwa ajili ya kuzalisha dawa zinazotumia mionzi, ni moja ya mifano hiyo ya kuweza taifa la Iran kusoma njama za maadui na kukabiliana nazo kiusomi na kiuelewa, jambo ambalo inabidi lishuhudiwe pia katika masuala yote ya nchi.
Vile vile amelitaja suala la ubunifu na kuwa mstari wa mbele katika kazi za kivitendo, kuwa ni jukumu kubwa la kimaadili na la busara la watu serikali, watu wa viwanda, wakulima, wawekezaji, wajasiriamali, watafiti wabunifu wa masuala ya kielimu na kiviwanda, wahadhiri wa Vyuo Vikuu, wakuu wa masuala ya kiuchumi na vituo vingine vya kielimu na kiteknolojia na kuongeza kuwa: Jukumu la watu wote ni kuwa waifanye nchi iwe madhubuti sana kiasi kwamba adui asiweze kujipenyeza ndani yake kwa hali yoyote ile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Suala hilo ni miongoni mwa mambo yanayohitajiwa na uchumi wa kimuqawama na kimapambano.
Nukta ya pili ambayo Ayatullah Udhma Khamenei ameiashiria katika sehemu hiyo ya hotuba yake ni ujumbe wa mara kwa mara unaotolewa na viongozi wa Marekani wa kutaka kuwa na mazungumzo kati yao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa: Wamarekani kwa muda sasa wamekuwa wakitumia njia mbali mbali kutoa ujumbe kuwa wanataka kufanya mazungumzo ya peke yao na Iran kuhusu suala la nyuklia la Iran, lakini mimi kutokana na uzoefu wa huko nyuma, sina imani na sina mtazamo mzuri na mazungumzo kama hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kwa mtazamo wa Wamarekani, mazungumzo hayana maana ya kufikia kwenye njia ya kimantiki na kuongeza kuwa: Kwa mtazamo wa Wamarekani, mazungumzo maana yake ni kuulazimisha upande wa pili ukubaliane na matakwa yao. Hivyo sisi siku zote tunayahesabu mazungumzo kama hayo kuwa ni mazungumzo ya kutwishwa na kuburuzwa; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haiko tayari kukubali kuburuzwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwa mara nyingine kuwa hana imani na mazungumzo kama hayo na kuongeza kwamba: Tab'an pamoja na hayo, mimi sina pingamizi yoyote.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumza kwa uwazi masuala kadhaa kuhusu Wamarekani.
Maudhui ya kwanza kuashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu jambo hilo, ni ujumbe mbali mbali wa mara kwa mara unaotolewa na Wamarekani wakidai kuwa hawana nia ya kuupindua utawala wa Iran.
Ayatulla Udhma Khamenei amesisitiza kuhusu suala hilo kuwa: Sisi kamwe hatukuwa na hofu na lengo lenu la kutaka kuupindua mfumo wetu wa Jamhuri ya Kiislamu, kwani tangu ule wakati ambapo mlikuwa na nia hiyo na mkawa mnaitangaza waziwazi, hamkuweza kufanya chochote na baada ya hapa pia hamtaweza kufanya chochote.
Vile vile ameashiria maudhui ya pili yaani sisitizo la Wamarekani la kwamba ni wakweli na wana nia nzuri katika pendekezo lao la mazungumzo na Iran na kusema kuwa: Sisi tumesema mara nyingi kuwa, hatuna nia ya kutengeneza silaha za nyuklia lakini Wamarekani wanasema bila ya kificho kuwa hawatuamini. Katika hali kama hiyo, vipi sisi tutaamini maneno ya Wamarekani wanapodai kuwa wana nia nzuri na ni wakweli katika pendekezo lao la kutaka mazungumzo na Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mtazamo na imani yetu sisi ni kuwa pendekezo hilo la mazungumzo ni ujanja tu wa Wamarekani na lengo la njama hizo ni kutaka kuzipotosha fikra za walio wengi duniani na kutaka kuwadanganya wananchi wa Iran na kama si hivyo, basi Wamarekani wanapaswa kuthibitisha kinyume chake kivitendo.
Katika sehemu hiyo ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria hila na ujanja mwingine unaotumika katika propaganda za Wamarekani kuhusu suala hilo na kusema kuwa: Kuna wakati Wamarekani walieneza propaganda kuwa kuna baadhi ya watu walioteuliwa na Kiongozi wa Iran ambao wanafanya mazungumzo na Marekani wakati ambapo maneno hayo ni uongo ulio wazi na hadi hivi sasa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuteuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Marekani.
Ameongeza kuwa: Katika masuala machache tu na kwenye baadhi ya masuala ya muda mfupi, serikali tofauti za Iran zimewahi kufanya mazungumzo na Marekani na hata katika mazungumzo hayo serikali hizo ziliwajibishwa kuchunga vizuri mstari mwekundu wa Kiongozi Muadhamu na leo hali ni hiyo hiyo, inabidi mistari myekundu ya taifa ichungwe kikamilifu.
Maudhui ya tatu ambayo imeashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na Marekani ni kutopenda Wamarekani kufikia kwenye natija nzuri mazungumzo hayo au kumalizika mazungumzo yanayohusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama Wamarekani wanataka kweli kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran, basi njia yake ni rahisi sana na wanapaswa kukiri haki ya Iran ya kurutubisha urani kwa malengo ya amani.
Aidha amekumbusha kuwa, kutekelezwa sheria ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA nakko unaweza kuondoa wasiwasi uliopo na kuongeza kuwa: Uzoefu na hali halisi ya mambo ilivyo inaonesha kuwa Wamarekani hawana nia ya kutatua suala la nyuklia la Iran na wanataka suala hilo libakie milele ili uwe wenzo wa kuliweka chini ya mashinikizo taifa la Iran na kwa ndoto zao waweze kulifanya kilema taifa hili, lakini maadui watakufa na ndoto zao hizo za kutaka kulifanya kilema taifa la Iran.
Nukta ya mwisho iliyozungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu suala hilo, ni kuwaonesha njia Wamarekani ya kuweza kutatua masuala yaliyopo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama Wamarekani wanataka kweli kutatua masuala yaliyopo, basi pendekezo letu la kuweza kutatua masuala hayo ni kuacha Wamarekani uadui wao dhidi ya taifa la Iran, kwa maneno na kwa matendo.
Vile vile amekumbushia siasa za kiuadui za Marekani dhidi ya taifa la Iran katika kipindi cha miaka 34 yaliyopita na kufeli siasa hizo na kuongeza kuwa: iwapo siasa hizo zitaendelea, basi zitashindwa tu kama zilivyoshindwa huko nyuma.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia suala muhimu sana la uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaotarajiwa kufanyika Juni 14 mwaka huu na kusema kuwa: Uchaguzi ni dhihirisho la hamasa ya kisiasa na nguvu za mfumo wa Kiislamu na irada ya taifa na heshima ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi huo kuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa na kusisitiza kuwa: Kushiriki kwa wingi na kwa hamasa kubwa wananchi katika uchaguzi huo sambamba na kudhamini usalama wa nchi, kutapelekea pia kutokuwa na athari vitisho vya maadui na kutawakatisha tamaa kabisa.
Vile vile amesisitiza juu ya udharura wa kushiriki watu wa mirengo yote na wenye mitazamo tofauti katika uchaguzi huo na kusisitiza kuwa: Uchaguzi hauwahusu watu wa mrengo mmoja na wa fikra moja tu, bali ni jukumu na ni haki ya watu wote wenye uchungu na nchi na wanaojali manufaa ya taifa na uhuru wa nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kuna baadhi ya wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ambao wanaweza kutumia vibaya fursa ya uchaguzi huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwa mara nyingine kuwa kura za wananchi ndizo zitakazoainisha mshindi na kuongeza kwamba, uamuzi wa wananchi juu ya nani bora zaidi kati ya wagombea ni jambo muhimu na wananchi wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu wagombea ili waweze kupata utulivu wa moyo kuhusu mtu anayefaa zaidi kwa ajili ya kumpa dhamana ya kubeba jukumu hilo.
Vile vile amesisitiza kuwa yeye hana zaidi ya kura moja tu katika uchaguzi na hakuna mtu yeyote atakayejua kura yake inakwenda kwa nani na kuongeza kuwa: Matamshi na maoni yoyote yale kuhusiana na kwamba Kiongozi Muadhamu anamuunga mkono mgombea fulani kuliko wagombea wengine kwa kweli ni maneno ambayo hayana ukweli wowote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia wananchi akiwaambia: Kuweni macho yasije masuala ya pembeni yakakuathirini katika kuchagua mtu anayefaa zaidi na msije mkatekwa na matamshi yanayotolewa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ikiwa ni pamoja na wimbi kubwa la ujumbe mfupi uliojaa katika zama hizi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza juu ya ulazima wa watu wote kuheshimu sheria na kuongeza kuwa: Matukio ya mwaka 1388 (Hijria Shamsia sawa na 2009 Milaadia) yalitokea kutokana na baadhi ya watu kukataa kuwa chini ya sheria na kuheshimu kura za wananchi na katika upande wa pili wakawachochea watu wafanye fujo mitaani makosa ambayo kwa hakika hayawezi kufutika kabisa.
Ameongeza kuwa: Kwa bahati nzuri sheria za nchi ziko kwa namna ambayo zina uwezo wa kuondoa utata wowote unaojitokeza, hivyo watu wote wana wajibu wa kuheshimu chaguo la wananchi walio wengi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu sifa anazopasa kuwa nazo rais anayekuja akisema kuwa: Rais anayekuja wa Iran anapaswa sambamba na kuwa na sifa za Rais aliyemtangulia, awe mbali pia na udhaifu aliokuwa nao Rais huyo wa kabla yake.
Ayatulla Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Inabidi chaguo la wananchi katika uchaguzi ujao wa Rais lioneshe kuweko maendeleo na kukamilika zaidi na liwe chaguo bora zaidi kuliko machaguo yote bora yaliyotangulia na hilo linatakikana katika kila kipindi cha uchaguzi.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Watu wanaoingia kwenye uchaguzi wa Rais wanapaswa wawe wanafungamana na Mapinduzi ya Kiislamu na matukufu ya Jamhuri ya Kiislamu, washikamane na manufaa ya taifa na wawe ni watu wanaoamini wajibu wa kuendeshwa nchi kimantiki, kushirikishwa watu wote na kwa umakini wa hali ya juu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Waiz Tabasi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala katika mkoa wa Khorasan Razavi na mdhamini wa Haram Tukufu ya Imam Ridha AS amemkaribisha Kiongozi Muadhamu na wafanya ziara wengine na huku akiashiria kaulimbiu ya mwaka huu wa Kiirani wa 1392 Hijria Shamsia amesema: Katika mwaka huu wa "Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi" wananchi walio macho na wenye mtazamo wa mbali wa Iran wataweza kupata mafanikio makubwa katika nyuga tofauti za kisiasa na kiuchumi na kwamba wataweza kutatua matatizo yao kwa juhudi, umoja, kupendana na kushirikiana.
1206471
captcha