Waandamanaji hao wameitaka jamii ya kimataifa kufanya jitihada za kusitisha mauaji ya Waislamu nchini Myanmar.
Wakati huo huo kiongozi wa Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar amesema kuwa serikali ya nchi hiyo inaeneza uchochezi na propaganda chafu dhidi ya Waislamu nchini humo.
Tun Khin ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waislamu wa Rohingya nchini Uingereza ameviambia vyombo vya habari kwamba mashambulizi yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhin yamesababisha vifo vya Waislamu wengi wa Rohingya na kuwalazimisha wengine zaidi ya laki moja kuwa wakimbizi ambao sasa wanaishi katika kambi zisizokuwa na huduma za aina yoyote.
Tun Khin amesema kuwa inasikitisha kwamba serikali ya Myanmar haiwalindi Waislamu mbele ya mashambulizi ya Mabudha na imekuwa ikifanya uchochezi na propaganda chafu dhidi yao. Amesisitiza kuwa uchochezi na propaganda chafu dhidi ya Waislamu zinaongezeka siku baada ya siku hata ndani ya bunge la Myanmar.
Maelfu ya Waislamu wameuawa kinyama na wengine wengi kukimbilia nje ya nchi kutokana na wimbi la mauaji yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wakishirikiana na askari wa jeshi la serikali ya Myanmar. 1208194