IQNA

Kiongozi wa al-Huthi asisitiza kuhusu umoja wa Waislamu

11:13 - January 05, 2015
Habari ID: 2672152
Kiongozi wa Harakati ya al-Huthi nchini Yemen, ametaka kulindwa umoja kati ya makundi ya kisiasa na kuwepo makubaliano na mshikamano wa kitaifa katika kukabiliana na njama za kigeni kwa ajili ya kutoa pigo kwa umoja nchini Yemen.

Sheikh Abdul-Malik Badreddin al-Houthi, aliyasema hayo mjini Sana'a Jumamosi kwa mnasaba wa kuanza sherehe za kuzaliwa Mtukufu Mtume Muhammad SAW, zinazosadifiana na kuanza kwa Wiki ya Umoja kati ya Waislamu. Akihutubia mkusanyiko mkubwa wa wananchi wa Yemen, Sheikh al-Houthi alisema: "Ujumbe wetu kwa nchi za Kiarabu na kieneo, ni kudumishwa amani, kuheshimiana, ujirani mwema na kutoingilia masuala ya ndani ya Yemen." Vile vile kiongozi huyo wa Harati ya al-Huthi alitaka kutatuliwa kwa uadilifu suala la kusini mwa Yemen na kuonya juu ya kutogeuzwa suala hilo kama wenzo wa kufikia malengo maovu. Sheikh Abdul-Malik al-Houthi aliashiria mpango wa kuifanya Yemen kuwa majimbo sita na kusema kuwa, mpango huo ni njama za mwisho zilizofeli za kutaka kuigawa nchi hiyo ya Kiarabu. Aidha amesema, kuzaliwa Mtukufu Mtume Muhammad SAW ni fursa bora kwa ajili ya umoja wa umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa, mataifa ya Kiislamu leo hii yanasisitizia zaidi suala la uhuru na kulindwa heshima na hadhi yao. Kiongozi wa Harakati ya al-Huthi nchini Yemen aliutaka umma wa Kiislamu sambamba na kulinda umoja, kuifanya Palestina kuwa kadhia kuu ya ulimwengu wa Kiislamu na kukabiliana na hatari inayolikabili eneo la Mashariki ya Kati hususan njama za makundi ya kitakfiri. Aligusia ongezeko la makundi ya kigaidi katika eneo hili na kusema, maadui wa Uislamu wameyaanzisha makundi hayo ili kuchafua sura halisi ya Uislamu. Hii ni katika hali ambayo duru za usalama nchini Yemen zimeripoti kujiri mauaji dhidi ya wanachama wa harakati ya al-Huthi katika mapigano na watu wenye silaha katika mji wa Ibb kusini mashariki mwa mji mkuu Sana'a. Kwa upande mwengine, watu wawili wameuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika shambulizi la watu wenye silaha dhidi ya gari moja aina ya basi katika mji wa Aden, kusini mwa Yemen. Aidha mapigano ya jeshi la nchi hiyo na watu wa makabila yanayobeba silaha katika mkoa wa Ma'rib huko mashariki mwa Yemen yamepelekea kwa akali watu 10 kuuawa. Hii ni katika hali ambayo Wizara ya Mambo ya Ndani pia imetangaza kuwa, askari wa nchi hiyo wamefanikiwa kuwatia mbaroni raia watatu kwa tuhuma za kushirikiana na kundi la kigaidi la al-Qaida, mmoja wao akiwa ni raia wa Ubegiji na mwengine kutoka Bulgaria huku mwengine akitoka Somalia na kwamba raia hao walitiwa mbaroni katika eneo la Sab'aain mjini Sana'a. Itakumbukwa kuwa baada ya mabadiliko yaliyojiri hapo mwaka 2011 nchini Yemen, kundi la kigaidi la al-Qaida lilishadidisha harakati zake ili kuidhoofisha serikali kuu na wakati huo huo kujiimarisha na kuongeza operesheni zake za kigaidi nchini humo. Mbali na hayo raia wa Yemen wanasisitizia ulazima wa kung'olewa utawala wa kidikteta nchini humo. Baada ya kutiwa saini makubaliano ya kugawana madaraka kati ya makundi ya kisiasa, nchi za Saudia, Marekani na Uingereza ziliamua kuikatia misaada nchi hiyo kama njia ya kukabiliana na Harakati ya Answarullah ambayo ndio yenye ushawishi mkubwa nchini humo hivi sasa. Hii ni katika hali ambayo Saudia bado inaendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Yemen.../mh

2672031

captcha