IQNA

Hujuma dhidi ya Misikiti kadhaa nchini Ufaransa

14:03 - January 12, 2015
Habari ID: 2700801
Stephen Le Foll, Msemaji wa serikali ya Ufaransa ametembelea na kukagua msikiti ulioko katika eneo la Port- la- Nouvelle kusini mwa nchi hiyo. Taarifa zinasema kuwa, msikiti huo ulishambuliwa kwa maguruneti matatu.

Taarifa zimeongeza kuwa, moja kati ya maguruneti hayo liliripuka msikitini, ingawa halikusababisha maafa kwa muumini yeyote msikitini humo. Wakati huohuo, msikiti mwingine ulioko katika eneo la Aude umeshambuliwa kwa kufyatuliwa risasi na watu wenye silaha. Wakati hayo yanajiri, mripuko wa bomu umetokea mapema leo mbele ya msikiti ulioko katika eneo la Rhone nchini humo. Mripuko mwingine umetokea mapema leo karibu na msikiti ulioko katika eneo la Villefranche-sur-Saone, lililoko mashariki mwa Ufaransa.

Duru za habari zinasema kuwa, tukio hilo limesababisha hasara kubwa kwenye mgahawa mmoja ulioko karibu na msikiti huo. Kwa upande mwingine, Bernard Perrut, Msaidizi wa Meya wa eneo la Villefranche - sur- Saone ameitaka serikali ya Ufaransa kuimarisha ulinzi na usalama zaidi kwenye misikiti kufuatia mashambulio ya mfululizo yaliyoilenga misikiti nchini humo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, jana lilifanyika shambulio la kigaidi dhidi ya ofisi ya jarida la kila wiki la Charlie Hebdo na kusababisha watu wasiopungua 12 kuuawa na wengine 10 kujeruhiwa.

Mwaka 2011, jarida la Charlie Hebdo liliwahi kuchapisha mara kadhaa vibonzo na vikatuni vinavyomvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw), na kuamsha hasira za Waislamu duniani kote.../mh

2699721

captcha