Kati ya wabunge hao Waislamu waliochaguliwa , nane ni wanawake. "Hizi ni habari nzuri kuwa kuna idadi kubwa ya wabunge Waislamu kuliko miaka iliyotanguliwa. Pamoja na hayo Bunge la Uingereza -House of Commons- bado haliakisi anuai ya watu wa matabaka na kaumu mbali mbali," amesema mhariri ya jarida la Muslim News, Ahmed J Versi. Ameongeza kuwa ni ishara nzuri kuona wanawake Waislamu zaidi wamechaguliwa mwaka huu ambapo sita kati yao ni wa chama cha Leba, moja ni chama cha Wahafidhina (Conservative) na mwingine wa Chama cha Kitaifa cha Uskochi SNP.
Bi. Tasnmina Ahmed Sheikh amekuwa mbunge wa kwanza Mwislamu wa SNP na amechaguliwa kwa ushindi wa kishindo katika eneo la Scotland huku Bi. Nusrat Ghani akiwa mbunge wa kwanza mwanamke Mwislamu katika chama cha Wahafidhina.
Pamoja na kuwa chama cha Leba kimepata pigo katika uchaguzi huo wa bunge siku ya Alkhamisi nchini Uingereza lakini wabunge wanne wapya Waislamu wamekipatia chama hicho kikuu cha upinzani viti vipya huku wengine watano wakifanikiwa kutetea viti vyao. Anas Sarwar wa Glasgow Scotland ndie mbunge pekee Mwislamu ambaye hakuweza kutetea kiti chake kutokana na ushindi mkubwa wa chama cha SNP.
Ushindi uliowashangaza wengi ni wa mwanaharakati wa afya ya kiakili Bi. Nasneem Shah ambaye ameshinda kiti cha Bradford Magharibi kwa tiketi ya chama cha Leba kwa kura 11,420 dhidi ya mgombea mashuhuri wa chama cha Respect George Galloway aliyepata kura 8,557 pamoja na kuwa alipata kupata ushindi wa kishindi katika uchaguzi mdogo wa mwaka 2012.
Kwa ujumla ni kuwa chama cha Leba kimepata wabunge tisa Waislamu chama cha Wahafidhina au Tories wabunge watatu Waislamu huku SNP kikipata mbunge moja Mwislamu.
Inafaa kuashiria hapa kuwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Bunge la Uingereza uliofanyika Alkhamisi yanaonyesha kuwa chama cha Wahafidhina kimepata ushindi mkubwa; na kwa utaratibu huo Waziri Mkuu David Cameron ataendelea kushika wadhifa huo kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa, chama cha Wahafdihina kimejinyakulia viti 331, chama cha Leba kimepata viti 232, Chama cha Kitaifa cha Uskochi (SNP) kimepata viti 56, na chama cha Demokrasia ya Kiliberali kimeambulia viti vinane. Viti vilivyosaliwa vimechukuliwa na vyama vidogo vidogo. Katika uchaguzi huo maelfu ya wagombea walichuana kuwania viti 650 vya bunge la Uingereza.../mh