Kundi hilo limetoa taarifa na kutangaza kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo la Ijumaa lililolenga waumini hao waliokuwa katika msafara wa kutembea kwa miguu kutoka mji wa Kanu kuelekea Zaria kushiriki kwenye kumbukumbu ya maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein (AS). Watu 22 waliuawa shahidi na wengine 38 walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea kwenye kijiji cha Dakasoye kilichoko umbali wa kilomita 20 kusini mwa mji wa Kano.
Ali Kakaki, mmoja wa waandalizi wa msafara huo amesema licha ya shambulio hilo la kigaidi, wameendelea na msafara wao wa kutembea kwa miguu na kwamba wanachama wengine wengi wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamejiunga na msafara huo. Ameongeza kuwa wanatarajia kuwasili mjini Zaria wiki ijayo kushiriki kwenye arubaini ya Imam Hussein AS. Ikumbukwe kuwa takribani miaka 1376 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) akiwa na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi za siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeshafanya mashambulio kadhaa kuwalenga Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria. Kundi hilo lenye ufahamu potofu kuhusu Uislamu limekuwa likishambulia pia Waislamu wa Kisuni na hata Wakristo nchini humo.