IQNA

Kiongozi Muadhamu kwa vijana Wamagharibi

Amilianeni kwa njia sahihi na ulimwengu wa Kiislamu

22:41 - November 29, 2015
Habari ID: 3458401
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amewaandikia barua vijana wa nchi za Magharibi akisema kuwa, matukio machungu ya kigaidi yaliyotokea nchini Ufaransa yameandaa uwanja wa kutafakari kwa pamoja kuhusu njia ya utatuzi wa migogoro ya sasa.

Amebainisha mifano ya kuhuzunisha ya athari mbaya za ugaidi unaoungwa mkono na baadhi ya madola makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, uungaji mkono wao kwa ugaidi wa kiserikali wa Israel na mashambulizi ya kijeshi yaliyosababisha hasara kubwa katika nchi za Waislamu kwenye miaka ya hivi karibuni na kuwaambia vijana kwamba: Ninawataka nyinyi vijana, mjenge nguzo za kuamiliana kwa njia sahihi na kiungwana na ulimwengu wa Uislamu kwa msingi wa utambuzi sahihi, uoni mpana na kwa kutumia tajiriba chungu.
Barua kamili ya Kiongozi Muadhamu kwa vijana wa nchi za Magharibi ni hii ifuatayo:

Kwa Jina la Allah Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu

Matukio machungu ambayo yamesababishwa na ugaidi mpofu nchini Ufaransa kwa mara nyingine yametufanya tuzungumze na nyinyi vijana. Ni jambo linalonisikitisha mimi matukio kama haya kuwa msingi wa hutuba yangu lakini ukweli wa mambo ni kuwa, iwapo masuala machungu hayatachukuliwa kuwa msingi wa kufikiriwa njia za utatuzi na kuwa chombo cha fikra za pamoja, bila ya shaka hasara itakuwa maradufu. Machungu ya kila mwanadamu katika kila pembe ya dunia, huwatia huzuni wanadamu wenzake. Mandhari ya mtoto anayekata roho mbele ya wapendwa wake, mama ambaye furaha ya familia yake hubadilika na kuwa maombolezo, mume ambaye hubeba mwili usio na roho wa mkewe na kuupeleka halahala sehemu fulani au mtazamaji ambaye hajui kuwa dakika chache zijazo huenda zikawa sehemu ya mwisho ya filamu ya maishani (humu duniani), ni mandhari zinazoathiri hisia za mwanadamu. Kila mtu ambaye amenufaika na mahaba na ubinadamu ataathirika na kuumizwa kwa kuyashuhudia matukio haya popote yanapotokea, yawe yanatokea nchini Ufaransa, Palestina, Iraq, Lebanon au Syria. Hapana shaka kuwa Waislamu bilioni moja na nusu wana hisia hiihii na wanachukizwa na kukerwa na watekelezaji wa maafa hayo. Ama suala muhimu hapa ni hili kwamba, iwapo machungu ya leo hayatapelekea kujengwa kesho iliyo bora na iliyo na amani zaidi, yatabakia tu kuwa kumbukumbu za matukio machungu na yasiyo na faida yoyote. Mimi ninaamini kuwa, ni nyinyi tu vijana ndio mnaoweza kujifunza kutokana na misukosuko ya leo ili kuweza kubuni njia za kujenga mustakbali na kuzuia upotovu ambao umewafikisha Wamagharibi walipo hivi sasa.
Ni kweli kuwa ugaidi leo umekuwa machungu ya pamoja kati yetu na nyinyi, lakini ni muhimu mfahamu ya kuwa, ghasia na wasiwasi ambao mmeupitia katika matukio ya hivi karibuni, una tofauti mbili muhimu na machungu ambayo watu wa Iraq, Yemen, Syria na Afghanistan wamekuwa wakiyapitia kwa miaka mingi. Tofauti ya kwanza ni kuwa, ulimwengu wa Kiislamu umekuwa mhanga wa unyama, hofu na ghasia kubwa zaidi na kwa muda mrefu sana na pili ni kwamba, kwa masikitiko makubwa, ghasia hizo zimekuwa zikichochewa na kuungwa mkono na madola makubwa na kwa njia tofauti na zenye taathira. Hii leo ni watu wachache mno ambao hawana habari kuhusiana na nafasi ya Marekani katika kubuni au kuimarisha na kuipa silaha al-Qaida, Taliban na makundi mengine maovu yanayofungamana na makundi hayo. Mbali na hayo uungaji mkono wa moja kwa moja na watoaji himaya wa wazi na wanaojulikana wa utakfiri, licha ya kuwa na mifumo iliyobaki nyuma kisiasa, lakini daima wanahesabiwa kuwa washirika muhimu wa nchi za Magharibi na hii ni katika hali ambayo fikra bora na zilizo wazi zaidi zinazotokana na uungaji mkono thabiti wa wananchi (demokrasia) katika eneo (Mashariki ya Kati) zinakandamizwa bila huruma. Miamala ya kindumakuwili ya Magharibi kuhusiana na mwamko kama huu katika ulimwengu wa Kiislamu ni mfano wa wazi wa mgongano uliopo katika siasa za Magharibi.
Mfano mwingine wa mgongano huo unaonekana katika kuunga mkono ugaidi wa serikali ya Israel. Ni zaidi ya miaka 60 sasa tokea wananchi madhlumu wa Palestina waanze kusulubiwa kwa aina mbaya zaidi ya ugaidi. Ikiwa watu wa Ulaya hivi sasa kwa siku kadhaa wamekuwa wakijificha kwenye nyumba zao na kujiepusha kushiriki kwenye mikusanyiko na vituo vilivyo na umati mkubwa wa watu, ni kwa makumi ya miaka sasa ambapo familia za Kipalestina hazina usalama hata ndani ya nyumba zao kutokana na mashine ya mauaji na uharibifu ya utawala wa Kizayuni. Leo ni utumiaji mabavu upi unaoweza kulinganishwa na unyama unaotekelezwa kupitia ujenzi wa vitongoji vya utawala wa Kizayuni? Bila ya kukabiliwa na aina yoyote ile ya ukosolewaji na ukemeaji wa maana kutoka kwa washirika wake walio na ushawishi mkubwa au kwa uchache taasisi za kimataifa ambazo kidhahiri zinaonekana kuwa huru, utawala huo kila siku hubomoa nyumba za Wapalestina na kutokomeza mabustani na mashamba yao bila hata kuwapa fursa ya kuondoa humo suhula na vyombo vyao wanavyovitumia maishani wala mazao yao ya kilimo. Aghlabu unyama huo hufanyika mbele ya macho yanayobubujika machozi ya watoto na wanawake walioingiwa na hofu kubwa ambao hushuhudia jamaa zao wakipigwa na kujeruhiwa na mara nyingine kupelekwa kwenye jela za kuogofya na za mateso (za Wazayuni). Je, mnajua ukatili mwingine mkubwa kama huu na katika zama hizi na wa muda mrefu katika sehemu nyingine yoyote ya dunia ya leo? Kuuawa kwa risasi mwanamke barabarani kwa kisingizio cha kumlalamikia askari aliyejizatiti vilivyo kwa silaha, kama si ugaidi huo basi ni nini? Je, kwa kuwa ukatili huu unafanywa na wanajeshi wa utawala vamizi haupasi kuitwa kuwa ni uchupaji mipaka? Au kwa vile picha hizi zimekuwa zikionyeshwa na kukaririwa kwenye televisheni kwa miaka 60, hazipasi tena kuchochea hisia zetu?
Kupelekwa kwa majeshi (ya nchi za kigeni) katika miaka ya hivi karibuni katika ulimwengu wa Kiislamu ambako kumechukua wahanga wengi, ni mfano mwingine wa mantiki inayogongana ya Magharibi. Nchi zinazohujumiwa mbali na kupata hasara za kibindamu, zimepoteza pia miundombinu yao ya kiuchumi na kiviwanda, harakati zao za maendeleo na ustawi zimesimama au kupungua kasi na hata katika baadhi ya sehemu zimerejea nyuma kwa makumi ya miaka. Licha ya hayo na kwa kiburi, nchi hizo zinatakiwa zisijihesabu kuwa ni nchi zinazodhulumiwa. Je, ni vipi nchi ambazo zimeharibiwa kwa kiwango hiki na miji na vijiji vyao vimefanywa jivu zitaambiwa: Tafadhali msijihesabu kuwa mliodhulumiwa?! Badala ya kutolewa wito wa kutofahamu au kusahau maafa, je, si bora kuomba msamaha wa dhati? Machungu ambayo yameupata ulimwengu wa Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni kutoka kwa wahujumu walio na nyuso mbili na zilizorembwa si madogo kuliko hasara ya kimaada.
Vijana wapenzi! Ninatumai kuwa nyinyi hivi sasa au katika siku zijazo mtaweza kubadilisha mtazamo na fikra hii potovu, fikra ambayo usanii wake ni kuficha malengo ya muda mrefu na kupamba malengo ya kuudhi. Kwa mtazamo wangu hatua ya kwanza ya kuleta usalama na utulivu, ni kurekebisha fikra hii ya kutumia mabavu. Maadamu vipimo vya kindumakuwili vitadhibiti na kughilibu siasa za Magharibi, kugawanywa ugaidi na waungaji mkono wake wenye nguvu katika makundi mawili ya ugaidi mzuri na mbaya, na maslahi ya serikali kufadhilishwa na kuwekwa mbele ya thamani za kiutu na maadili, basi mizizi ya utumiaji mabavu haipasi kutafutwa kwingine.
Inasikitisha sana kuwa mizizi hii, katika kipindi cha miaka mingi, pia imejikita hatua kwa hatua katika sera za kiutamaduni za Magharibi na kuandaa hujuma laini na ya kimya.
Nchi nyingi za dunia zinajifakharisha kwa utamaduni wao wa jadi na wa kitaifa; hizi ni tamaduni ambazo sambamba na kuinuka na kustawi, kwa mamia ya miaka zimekuwa zikikidhi vyema mahitaji ya jamii za mwanadamu. Ulimwengu wa Kiislamu nao pia hauko nje ya duara hili. Lakini katika zama zetu hizi, ulimwengu wa Magharibi unatumia suhula za kisasa ili kulazimisha kuwepo utamaduni unaoshabihiana na unaofanana kote duniani. Mimi ninaamini kuwa, kutwisha utamaduni wa Magharibi kwa mataifa mengine na kudunisha tamaduni huru ni utumiaji mabavu kimya na wenye madhara makubwa sana.
Mwenendo huu wa kudhalilisha tamaduni tajiri na kuvunjia heshima matukufu makubwa zaidi ya tamaduni hizo unafanyika katika hali ambayo, tamaduni mbadala hazina sifa na uwezo wa kuchukua nafasi ya tamaduni hizo. Kwa mfano, mambo mawili ya "ushari" na "ufuska na utovu wa maadili" ambazo, kwa masikitikio, zimekuwa misingi mikuu ya utamaduni wa Magharibi, zimepoteza nafasi hata hukohuko zilikozaliwa. Hapa swali linalojitokeza ni kwamba, je, tutakuwa watenda dhambi na makosa iwapo tutakataa utamaduni wenye kupenda machafuko, wa ufuska na usiokubali masuala ya kiroho? Je, tunakosea iwapo tutazuia mafuriko na uharibifu ambao unakuja kwa vijana wetu katika fremu ya bidhaa za kisanaa? Mimi sipingi umuhimu na thamani za mahusiano ya kiutamaduni. Mahusiano hayo yanapofanyika katika mazingira ya kawaida na kwa kuheshimu jamii husika huitunuku ustawi, maendeleo na kuitajirisha. Mkabala wake, mahusiano yasiyooana na ya kulazimishwa hayafanikiwi na husababisha hasara. Kwa masikitiko nalazimika kusema kwamba, makundi maovu kama Daesh ni wazaliwa na matokeo ya maingiliano kama hayo yasiyo na mafanikio na tamaduni kutoka nje. Kama kweli tatizo lingekuwa la kiitikadi basi tatizo hili pia lingeshuhudiwa katika ulimwengu wa Kiislamu kabla ya zama za ukoloni, hata hivyo historia inathibitisha kinyume chake. Nyaraka za kuaminika za kihistoria zinaonesha waziwazi jinsi muungano wa ukoloni na fikra za kuchupa mipaka na zisizokubalika tena ndani ya kabila moja la kibedui, ulivyopandikiza mbegu ya misimamo mikali katika eneo hili. La sivyo inawezekana vipi kutokea taka kama Daesh katika mojawapo ya mifumo ya kidini yenye maadili zaidi na ya kibinadamu zaidi duniani ambao unasisitiza katika misingi na nguzo zake kwamba kutoa roho ya mwanadamu mmoja ni sawa na kuua wanadamu wote?
Katika upande mwingine inatupasa kuuliza kwamba, ni kwa nini watu waliozaliwa Ulaya na kupata malezi ya kifikra na kiroho katika mazingira hayo wakavutwa na kuathiriwa na makundi hayo? Je, inawezekana kuamini kwamba, watu hawa wamepata ghafla misimamo ya kuchupa mipaka kwa kufanya safari moja au mbili katika maeneo ya vita kiasi cha kuwafanya wawamiminie risasi wananchi wenzao? Bila ya shaka (katika mazingira kama haya) haiwezekani kusahau na kupuuza taathira za kipindi kirefu cha kulishwa utamaduni usio sahihi katika mazingira machafu na yanayozalisha ukatili. Tunapasa kuwa na uchambuzi kamili na wa pande zote, uchambuzi utakaobaini uchafu wa dhahiri na wa siri wa jamii. Inawezekana kwamba chuki kubwa iliyopandikizwa katika nyoyo za matabaka mbalimbali ya jamii za Magharibi kwa kipindi cha miaka mingi ya ustawi wa kiviwanda na kiuchumi na kutokana na dhulma na wakati mwingine ubaguzi wa kisheria na kimuundo, imezusha vinyongo ambavyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara kama maradhi katika sura hii.
Alaa kulli hal, sasa mnalazimika kuvunja tando za kidhahiri za jamii zenu, mupate na kuondoa vifundo na vinyongo vilivyomo. Nyufa zilizopo zinapaswa kurekebishwa badala ya kupanuliwa zaidi. Kosa kubwa katika kupambana na ugaidi ni kuchukua misimamo ya kukurupuka itakayozidisha mipasuko iliyopo. Harakati yoyote ya kijazba na ya kukurupuka ambayo itaitenga au kuitia hofu na katika misukosuko jamii ya Waislamu wa Ulaya na Marekani ambayo ina mamilioni ya watu wenye kujituma na kuwajibika, na ikapelekea kunyimwa zaidi haki zao za kimsingi na kuwaweka kando, si tu kwamba haitatatua tatizo, bali pia itapanua zaidi nyufa na kuzidisha vinyongo. Hatua za kijuujuu na misimamo ya kukurupuka hususan pale inapohalalishwa kisheria, mbali na kwamba haitakuwa na matokeo ghairi ya kuzidisha kambi zilizopo, vilevile itafungua njia ya migogoro mipya katika siku za usoni.
Habari zilizotufikia zinasema kuwa, katika baadhi ya nchi za Ulaya kumewekwa taratibu zinazowalazimisha raia kufanya ujasusi dhidi ya Waislamu. Mwenendo huu ni wa kidhalimu na sisi zote tunajua kwamba – kwa kupenda au bila ya kupenda - dhulma ina sifa ya mwangwi. Zaidi ni kwamba Waislamu hawastahiki utovu huo wa fadhila. Dunia ya Magharibi inawajua vyema Waislamu kwa karne nyingi. Wakati Wamagharibi walipokuwa wageni katika ardhi ya Uislamu na kukodolea macho utajiri wa mwenye nyumba, na vilevile wakati mwingine ambapo walikuwa wenyeji na wakafaidika na kazi na fikra za Waislamu, aghlabu hawakuona lololote kutoka (kwa Waislamu) isipokuwa ukarimu na uvumilivu.
Kwa msingi huo ninawataka nyinyi vijana, mjenge nguzo za kuamiliana kwa njia sahihi na kiungwana na ulimwengu wa Uislamu kwa msingi wa utambuzi sahihi, uoni mpana na kwa kutumia tajiriba chungu. Katika hali hiyo mutaona katika kipindi si kirefu kijacho, jengo mlilojenga juu ya nguzo hizo imara likiweka kivuli cha imani na kuaminiana juu ya vichwa vya wahandisi wa jengo hilo, kuwatunuku vuguvugu la amani na utulivu na hatimaye kumulika mwanga wa matumaini katika mustakbali wa dunia.
Sayyid Ali Khamenei
8/Azar/1394
(29/Novemba/2015 )

3458369

captcha