FAI imeidhinisha azimio rasmi la kuwasilisha ombi kwa UEFA ili kuiondoa Israel katika mashindano ya vilabu na timu za taifa barani Ulaya. Azimio hilo, lililopendekezwa na klabu ya Bohemians ya Dublin, limetaja ukiukaji wa vifungu viwili vya katiba ya UEFA unaofanywa na Shirikisho la Soka la Israel (IFA): kushindwa kutekeleza sera madhubuti dhidi ya ubaguzi wa rangi, na kuendesha vilabu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu bila idhini ya Shirikisho la Soka la Palestina.
FAI ilieleza kuwa azimio hilo liliungwa mkono kwa kura 74, huku saba wakilipinga na wawili wakijizuia kupiga kura. UEFA bado haijatoa tamko rasmi kuhusu hatua hiyo.
UEFA ilisitisha mipango ya kuifukuza Israel mwishoni mwa Septemba kufuatia tangazo la mpango wa 'amani' wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu eneo hilo.
Ingawa UEFA haikuthibitisha rasmi kuwa ilikuwa ikifikiria kuitisha kikao cha dharura cha kamati yake kuu kujadili suala hilo, taarifa zinaonyesha kuwa mipango hiyo ilikuwa imefikia hatua ya juu, na kikao kingeweza kuitishwa kwa haraka.
Kituo cha utangazaji cha kitaifa cha Ireland, RTÉ, kiliripoti kuwa FAI ilisema: “Katika mkutano mkuu wa dharura wa Shirikisho la Soka la Ireland, azimio la kawaida liliwasilishwa kwa wajumbe wa Bunge Kuu la FAI. Liliidhinishwa kwa wingi wa kura , 74 waliunga mkono, saba walipinga, wawili walijizuia.”
RTÉ iliongeza kuwa FAI imekusudia “kuwasilisha ombi rasmi kwa kamati kuu ya UEFA kuomba kusimamishwa mara moja kwa Shirikisho la Soka la Israel katika mashindano ya UEFA kutokana na kuvunja vifungu viwili vya katiba ya UEFA.”
Azimio hilo liliorodhesha ukiukaji huo kama: “kuendesha vilabu katika makazi haramu ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu bila idhini ya Shirikisho la Soka la Palestina, kinyume na katiba ya FUFA (Kifungu cha 73) na katiba ya UEFA (Kifungu cha 5)” na “kushindwa kwa IFA kutekeleza sera madhubuti dhidi ya ubaguzi wa rangi, kinyume na katiba ya UEFA (Kifungu cha 7bis).”
Hatua ya Ireland inafuatia miito iliyotolewa mwezi Septemba na viongozi wa mashirikisho ya soka ya Uturuki na Norway wakitaka Israel isimamishwe kushiriki mashindano ya kimataifa.
Miito hiyo ilikuja baada ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuomba FIFA na UEFA kuisimamisha Israel, wakinukuu ripoti ya tume ya uchunguzi ya UN iliyosema kuwa utawala wa Israel ulitenda jinai ya mauaji ya halaiki wakati wa vita vya Gaza.
Iwapo UEFA itaamua kuifukuza Israel, hatua hiyo itaiweka katika mgongano wa moja kwa moja na serikali ya Marekani, ambayo ni mwenyeji mwenza wa Kombe la Dunia la 2026, na inapinga vikali hatua hiyo. Ingawa UEFA ina mamlaka ya kuisimamisha Israel au vilabu vyake katika mashindano ya barani Ulaya, huenda isiweze kuizuia kushiriki katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, ambazo zinasimamiwa na FIFA.
3495324