
Ayatullah Makarim Shirazi, ameyasema hayo leo katika kongamano la kimataifa mjini Qum, kusini mwa nchi na kuongeza kwamba, udiplomasia na njia za kijeshi sio pekee za kuhitimisha janga hilo.
Amesema kukabiliana na hatari ya makundi yenye kuwakufurisha Waislamu wengine katika ulimwengu wa leo, ni jukumu la maulama wote wa Kiislamu. Ameongeza kuwa, maulama wa Kiislamu kwa pamoja wanatakiwa kushirikiana katika kung'oa mizizi ya utakfiri kifikra na hata kupitia vyombo mbalimbali vya upashaji habari. Amesisitiza kuwa, kongamano hilo la kimataifa linajitahidi kuchunguza chanzo cha fikra za utakfiri na kujibu fikra hizo kupitia majibu ya kimantiki ili kuweza kuwaepusha vijana kunako kuhadaiwa na magenge hayo. Marjaa huyo maarufu na mfasiri mkubwa wa Qur'an Tukufu amesema kuwa, maulama wa Kiislamu sanjari na kuyatenga mbali makundi ya kitakfiri na dini Tukufu ya Kiislamu, wanatakiwa pia kuutangazia ulimwengu wa Kiislamu kuwa Uislamu sio dini ya ukatili, umwagaji damu na uharibifu, bali ni dini ya upole na upendo. Aidha ameashiria mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, kuwafanya wakimbizi mamilioni ya watu, uharibifu wa misikiti, makaburi na athari za Kiislamu na uharibifu wa miundombinu ya nchi za Kiislamu kunakofanywa na makundi hayo na kusema, ushirikiano wa magenge hayo na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kimagharibi kwa ajili ya kuuteketeza Uislamu, ni mambo ambayo hii leo yamembainikia wazi kila mtu. Akiashiria kuwa, hii leo Uislamu unakabiliwa na hatari kubwa inayosababishwa na magenge hayo ya utakfiri amesema kuwa, hasara inayotokana na matakfiri ni kubwa zaidi kuliko inavyofikiriwa. Kongamano hilo limehudhuriwa na maulama mbalimbali wa madhehebu ya Sunni na Shia kutoka pembe mbalimbali za dunia mjini hapo Qum.