IQNA

"Ima kufa Shahidi au Uhuru" asema Mpalestina aliyegoma kula chakula gerezani Israel

6:41 - February 14, 2016
Habari ID: 3470135
Mohammad al Qiq mwandishi habari Mpalestina aliyegoma kula anakoshikiliwa katika jela ya Israel amekataa pendekezo la kuachiliwa huru kwa masharti.

"Msimamo wa Qiq uko wazi, anakataa pendekezo lololote ambalo halitajumuisha kusitishwa kushikiliwa kwake korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka. Aidha amesema akiachiliwa huru apate matibabu katika hospitali za Kipalestina," amesema afisa wa masuala ya wafungwa katika Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Amesema ana machaguo mawili tu ima aachiliwe huru bila masharti au afe shahidi.

Jumuiya ya Waandishi Habari Waislamu imetangaza mshikamano wake na mwandishi habari mateka wa Palestina anayeshikiliwa katika korokoro za utawala ghasibu wa Israel, Muhammad al Qiq.

Jumuiya ya Waandishi Habari Waislamu imelaani vikali jinai zinazoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Muhammad al Aqiq, mwandishi habari wa Palestina anayefanya mgomo wa kula akipinga ukatili na unyama wa Israel na kutangaza kuwa, Wazayuni wamezidisha ukatili na unyama wao dhidi ya taifa la Palestina kutokana na kukosekana idara ya kweli ya nchi za Magharibi na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Israel huko Palestina.


Taarifa ya Jumuiya ya Waandishi Habari Waislamu imezitaka jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu kufanya jitihada zaidi za komesha jinai na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jumuiya hiyo pia imeitaka jamii ya waandishi habari na wamiliki wa vyombo vya habari kutekeleza wadhifa wao wa kumtetea mwandishi huyo wa habari anayeshikiliwa mateka na wasiuruhusu utawala haramu wa Israel kutimiza ukatili wake chini ya mwavuli wa kimya cha nchi zinazodai kutetea demokrasia na haki za binadamu.

Muhammad al Qiq, mwandishi habari wa Palestina anayeshikiliwa katika korokoro za Israel alianza mgomo wa kula siku 80 zilizopita akipinga kukamatwa kwake bila na makosa yoyote. Madaktari wanasema hali ya mwandishi huyo wa habari wa Palestina ni mbaya sana.

Utawala haramu wa Israel unawashikilia Wapalestina 600 pasina kuwa kuwafungulia mashtaka. Kwa ujumla kuna Wapalestina elfu saba katika jela za kuogofya za utawala dhalimu wa Israel.

3459022

captcha