IQNA

Rais wa Kenya amtunuku nishani Mwalimu Mwislamu aliyenusuru Wakristo

15:00 - April 02, 2016
Habari ID: 3470225
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amemtunuku nishani ya juu Salah Farah marehemu mwalimu Mwislamu aliyepigwa risasi akiwakinga Wakristo wasiuawe na magaidi wa Al Shabab.

Akuhutubia taifa bungeni siku ya Alkhamisi mjini Nairobi, Rais Kenyatta alisema serikali yake itawatuza wale Wakenya wachache wanaoonesha ujasiri wa kukabiliana dhidi ya magaidi wa al Shabab.

Katika hotuba yake, Rais Kenyatta alisema, "Namtunuku marehemu Salah Farah nishani ya Order of the Grand Warrior of Kenya (nishani ya juu ya ushujaa Kenya). Alikuwa Mwislamu aliyepoteza maisha akiwakinda Wakristo. Nampongeza Farah, mwalimu ambaye alipoteza maisha akiwalinda Wakristo walipokuwa wakishambuliwa na al-Shabab."

Farah aliwakinga Wakristo dhidi ya kushambuliwa na wapiganaji wa kundi la magaidi wakufurishaji wa Al-Shabab waliovamia basi lililokuwa likielekea mjini Mandera mnamo Desemba 21 2015 kaskazini mashariki mwa Kenya.

Farah aliaga dunia tarehe 18 Januari alipokuwa akiendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta mjini Nairobi.

Farah aliyekuwa naibu mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Mandera Township, alisafirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi mwezi Desemba kwa ajili ya matibabu maalumu kufuatia shambulio hilo.

Abiria Waislamu walionyesha hatua ya kishujaa walipozuia mauaji ya halaiki walipowakinga wenzao Wakristo dhidi ya wapiganaji wa Al Shabab waliovamia basi lililokuwa na abiria 62 kati ya maeneo ya Dabacity na Borehole II.

Al-Shabab walikuwa wamevizia basi na lori zilizokuwa zinaelekea mjini Mandera kutoka Nairobi ambapo watu wawili waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa vibaya.

Abiria Waislamu walisimama kidete na kuwaambia Al Shabab kuua abiria wote la sivyo waondoke bila kumgusa hata mmoja.

Wanawake Waislamu waliwavika wenzao Wakristo na vazi la hijabu kwa lengo la kuchanganya magaidi hao dhidi ya kuwashambulia.

Farah alikuwa miongoni mwa abiria Waislamu waliojeruhiwa na Al-Shabaab walipokuwa wakijaribu kuwakinga Wakristo.

Waislamu walikataa kutenganishwa na wenzao Wakristo.

Baadaye wanamgambo hao wa Al-Shabab walitoroka baada ya kusikia mngurumo wa lori lililokuwa nyuma ya basi hilo lililokuwa likitoka Nairobi.

Siku ya Alkhamisi kabla ya hotuba yake bungeni, Rais wa Kenya alimpigia simu mjane wa Farah na kumhakikishia kuwa serikali itamsaidia yeye na watoto watano walioachwa na marehemu.


captcha