IQNA

Waislamu Kenya walaani mpango wa kubomoa msikiti Nairobi

0:22 - April 09, 2017
Habari ID: 3470925
TEHRAN (IQNA)-Waislamu nchini Kenya wameandamana kulaani mpango wa wakuu wa mji wa Nairobi kubomoa msikiti moja mjini humo kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Mamia ya Waislamu waliokusanyika baada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Jamia mjini Nairobi wametaja hatua ya Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara za Mijini (KURA), kutaka kuubomoa Msikiti wa City Park kuwa kinyume cha sheria. Wamesema hati miliki na stakabadhi za msikiti huo zilipatikana kwa njia halali mwaka 2005 na ujenzi kuanza baada ya idhini ya idara husika za baraza la mji.

Muweka hazina wa msikiti huo Abdulhamid Chaudry amesema Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara za Mijini Kenya (KURA) ilitoa ilani ya kutaka kuubomoa msikiti huo mwaka 2015 kwa madai kuwa umejengwa katika ardhi ya barabara na kwa msingi huo hakuna fidia yoyote itakayolipwa. Amesema hili ni jambo lisilokubalika na kwamba KURA inapaswa kuwalipa Waislamu fidia na kuwapa ardhi mbadala.

Chaudry amesema hivi sasa kuna uchunguzi wa umma unaoendelea katika Tume ya Kitaifa ya Ardhi Kenya (NLC) kuhusu mgogoro huo. "Tumeshtushwa na kuendelea kupuuzwa sheria na kuchelewesha kesi za ardhi." Ametaka mamlaka husika kusitisha mara moja ukiukwaji wa sheria sambamba na na kutoa wito wa kufanyika haki na uadilifu huku Waislamu wakisuburi kesi ya ardhi hiyo." Amebainisha masikitiko kuwa KURA inataka kuubomoa msikiti huo kabla ya kesi kumalizika.

Sheikh Salim Mohammed wa msikiti huo pia amesisitiza kuwa KURA inapaswa kuwalipa Waislamu fidia na kuwapa ardhi mbadala kwani msikiti unamiliki ardhi hiyo kihalali. Amesema msikiti huo huwahudumia Waumini 2,500 mbali na kuwa na Madrassah ambayo huwa na nafasi muhimu kuwafunza watoto maadili mema.

Hatahivyo kaimu mkurugenzi wa KURA Silas Kintori amesema mamlaka hiyo haina nia ya kuubomoa msikiti huo na kwamba inafanya mazungumzo na washikadau wote ili kutafutia suala hilo suluhisho bora.

Amesema tokea mwaka 2012, KURA imekuwa ikifanya mazungumzo na wahusika wote ikiwemo kamati ya msikiti kwa ajili ya kutafutia mgogoro huo suluhisho.

3462523

captcha