IQNA

Tafsiri mpya ya Qur’ani yachapishwa Algeria

19:07 - April 05, 2016
Habari ID: 3470228
Tafsiri ya kwanza ya Qur’ani katika zama hizi nchini Algeria imechapishwa kwa anuani ya Ad Darul Thamin Fi Tafsir al Quran na imeandikwa na Allamah At-Tawati bin At-Tawati.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, tafsiri hiyo ni ya kwanza kutayarishwa na kuchapishwa nchini Algeria katika zama hizi na kwamba imesambazwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Darul Hikmat nchini humo.

Katika tafsiri yake mpya ya Qur’ani Tukufu, Allamah At-Tawati amejaribu kutumia lugha sahali ili kuwawezesha watu wote wafaidike nayo. Tafsiri hiyo inatoa muongozo mpya katika kufahamu mafundisho ya Kiislamu.

Aidha katika tafsiri hiyo imezingatia msingi wa fiqhi linganishi na kwa mujibu wa mantiki pasina kuwepo taasubi kuhushu madhehebu za Kiislamu.

Allamah At-Tawati alizaliwa mwaka 1943 katika mji wa Laghouat nchini Algeria kusini mwa mji mkuu Algiers. Alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Mabrouk Kuwaisi na alisoma katika chuo kilichokuwa kinasimamiwa na Jumuiya ya Maulamaa Waislamu Algeria na kabla ya Algeria kujinyakulia uhuru mwaka 1962 alikuwa mwanachama wa Jeshi la Ukombozi wa Aljeria.

Mbali na Tafsiri, Sheikh At-Tawati ameandika vitabu vingi vya fiqhi, fiqhi linganishi na nahw .

Aidha ameandika kitabu cha jildi tano cha kifiqhi chenye anuani ya Al-Mubsit fi Al-Fiqh Al-Maliki bil-Adillah na vile vile kitabu kingine cha fiqhi linganishi chini ya anuani ya "Al-FiqhAl-Muqarin”.
3486070

captcha