Kwa mujibu wa muswada huo, adhabu ya kuvaa Niqabu hadharani itakuwa faini kati ya euro 200 hadi 4,000 (takriban Ksh 30,000 hadi 600,000). Aidha, mtu yeyote atakayemlazimisha mwingine kuvaa aina hiyo ya Hijabu anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka mitatu.
Hata hivyo, uvaaji wa Hijabu hiyo utaruhusiwa katika ndege, maeneo ya kidiplomasia, na sehemu za ibada.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, muswada huo sasa utajadiliwa na Kamati ya Bunge ya Masuala ya Katiba, Haki, Uhuru na Dhamana, chombo kinachohusika na kuchunguza sheria zinazogusa masuala ya kikatiba.
Iwapo muswada huo utasainiwa kuwa sheria, Ureno itajiunga na nchi nyingine za Ulaya kama Ufaransa, Austria, Ubelgiji na Uholanzi ambazo tayari zina marufuku kamili au ya sehemu kuhusu uvaaji wa vilemba vya uso.
Rais Marcelo Rebelo de Sousa bado anaweza kuupinga muswada huo au kuutuma kwa Mahakama ya Katiba kwa uchunguzi zaidi.
Wakati wa kikao cha bunge Ijumaa, kiongozi wa Chega, Andre Ventura, alikabiliwa na wabunge wanawake kutoka vyama vya mrengo wa kushoto waliopinga muswada huo. Hata hivyo, muswada ulipitishwa kwa msaada wa muungano wa vyama vya mrengo wa kati-kulia.
Ventura alisema: “Leo tunawalinda wabunge wanawake, binti zenu, binti zetu, dhidi ya kulazimika kuvaa burqa siku moja katika nchi hii.” Kupitia chapisho kwenye X (zamani Twitter), aliandika: “Leo ni siku ya kihistoria kwa demokrasia yetu na kwa kulinda maadili yetu, utambulisho wetu na haki za wanawake.”
Mbunge Andreia Neto kutoka chama tawala cha Social Democratic Party alisema kabla ya kura: “Hili ni mjadala kuhusu usawa kati ya wanaume na wanawake. Hakuna mwanamke anayepaswa kulazimishwa kufunika uso wake.”
Vyama viwili kati ya kumi bungeni vilijizuia kupiga kura, chama cha People-Animals-Nature na Together for the People, ambavyo vilieleza kuwa pendekezo hilo linaweza kuchochea ubaguzi.
Ni wachache tu miongoni mwa wanawake Waislamu barani Ulaya wanaofunika nyuso zao, na nchini Ureno, uvaaji wa vilemba hivyo ni nadra sana. Hata hivyo, mavazi kama niqab na burqa yamekuwa suala lenye utata barani Ulaya, ambapo baadhi ya watu hudai kuwa yanawakilisha ubaguzi wa kijinsia au tishio la kiusalama, hivyo yanapaswa kupigwa marufuku.
3495046