IQNA

Ushirikiano katika Qur’ani Tukufu/3

Ammri Nane za Ushirikiano Katika Qur'ani Tukufu

9:21 - October 19, 2025
Habari ID: 3481383
IQNA-Katika Aya ya pili ya Surah Al-Ma’idah, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaja amri nane muhimu, ambazo ni miongoni mwa maagizo ya mwisho aliyoteremshiwa Mtume Muhammad (Rehema na Amani zimshukie). Miongoni mwa amri hizo ni kushikamana kwa pamoja katika njia ya wema na uchamungu.

Aya hii inahusiana na ibada ya Hija na safari ya kwenda Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Inasisitiza kuwa ni wajibu kwa Waislamu kuheshimu alama zote za Mwenyezi Mungu, na ni haramu kuvunja heshima ya ibada hizo. Miongoni mwa alama zilizotajwa ni miezi mitakatifu, kafara, marufuku ya kuwinda ukiwa katika Ihramu, na heshima kwa mahujaji wanaoelekea kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Msivunje heshima ya alama za Mwenyezi Mungu.” Hii ni amri ya wazi ya kutotenda kinyume na ibada zilizoamrishwa na Mwenyezi Mungu.

Aya inaendelea kwa kuonya kuwa, baada ya ushindi wa Makka, Waislamu wasiruhusu chuki za zamani, kama vile kuzuia Hija mwaka wa sita Hijria, kuwapelekea kwenye uadui au mashambulizi. Mwenyezi Mungu anasema: “Na chuki ya watu fulani isikufanyeni muache kwenda Msikiti Mtakatifu wala isiwapelekee kwenye uadui.”

Ingawa amri hii ilihusiana na Hija, ujumbe wake ni wa jumla kwa maisha ya kila siku ya Muislamu. Muislamu hapaswi kuwa na kinyongo, kulipiza kisasi, au kufufua maovu ya zamani. Tabia hizi huleta unafiki na mgawanyiko katika jamii, jambo ambalo lilikuwa na uzito mkubwa katika siku za mwisho za Mtume Muhammad (SAW).

Katika aya inayofuata, Mwenyezi Mungu anatufundisha kuwa badala ya kushirikiana katika maovu au kulipiza kisasi, tunapaswa kushirikiana katika mambo ya kheri na uchamungu. Anasema: “Na shirikianeni katika wema na uchamungu, wala msishirikiane katika dhambi na uasi.”

Aya inahitimisha kwa kutuamrisha tuwe na taqwa—kumcha Mwenyezi Mungu—na kutotenda kinyume na amri Zake, kwani adhabu Yake ni kali. Mwenyezi Mungu anasema: “Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.”

3495015

Kishikizo: qurani tukufu MAWAIDHA
captcha