IQNA

Waziri wa Kizayuni Auhujumu Tena Msikiti wa Al-Aqsa

8:12 - October 18, 2025
Habari ID: 3481381
IQNA-Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni, licha ya onyo kutoka kwa Waqfu wa Kiislamu, ameuvamia tena Msikiti wa Al-Aqsa jijini Quds (Jerusalem) kwa mara ya pili ndani ya wiki moja.

uvamizi huo ulifanyika asubuhi ya Jumanne katika mji wa Quds uliokaliwa kwa mabavu, chini ya ulinzi mkali wa polisi wa utawala wa Kizayuni.

Idara ya Waqfu wa Kiislamu mjini Quds ilitoa taarifa fupi ikisema: “Ben Gvir leo asubuhi aliingia msikitini bila taarifa ya awali.” Hii ni kinyume na utaratibu wa kawaida ambapo mawaziri wa Israel hawaruhusiwi kuingia Msikiti wa Al-Aqsa bila idhini rasmi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Hii ni mara ya 13 kwa Ben Gvir kuvamia Msikiti tangu achukue wadhifa huo, ikiwa ni pamoja na uvamizi 10 tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023.

Kwa upande mwingine, Baraza la Waqfu na Masuala ya Kiislamu pamoja na Maeneo Matakatifu ya Quds limetangaza kuwa mwaka 2025 umeshuhudia uharibifu mbaya zaidi wa hali ya kidini na kisheria katika historia ya Msikiti wa Al-Aqsa.

Katika taarifa yake, baraza hilo limeeleza kuwa maafisa wa utawala wa Kizayuni na makundi ya misimamo mikali wameongeza uvamizi wao msikitini na kuwaruhusu walowezi wa Kizayuni kufanya ibada za Talmud katika viwanja vya msikiti huo.

Baraza hilo pia limelaani vikali uingiliaji wa maafisa wa utawala wa Kizayuni unaozuia miradi ya ukarabati wa Msikiti wa Al-Aqsa, pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wafanyakazi na walinzi wa waqfu.

Katika muktadha huo, Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Wahamiaji ya Jordan imelaani kwa maneno makali uvamizi wa Itamar Ben Gvir katika Msikiti wa Al-Aqsa, pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya Kiyahudi yenye misimamo mikali yanayoungwa mkono na polisi wa utawala wa Kizayuni.

Wizara hiyo, katika taarifa rasmi, imetaja kitendo hicho kuwa ni ukiukaji wa wazi wa hali ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa, ni dharau kwa utakatifu wa msikiti huo, na ni uchochezi hatari unaopaswa kulaaniwa. Aidha, imesisitiza kuwa uvamizi huo ni uchokozi usiovumilika dhidi ya hisia za Waislamu duniani kote.

4310788

Kishikizo: al aqsa wazayuni
captcha