IQNA

Mpango wa Tarjama ya Qur’ani kwa lugha ya Kiluhya ya Kenya

17:51 - April 06, 2016
Habari ID: 3470230
Wasomi watano Waislamu kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya wamezindua mpango wa kutayarisha Tarjama ya Qur’ani kwa lugha ya Kiluhya .

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, wasomi hao ni mabwana Harun Musa, Ramadan Sebwa, Ramadhan Ndege, Ismail Were na Yusuf Malala.

Sheikh Musa anasema alipata ilhamu akiwa gerezani Desemba mwaka 2014 kwa tuhuma za kuwa mfuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabab. "Nilihisi kuwa kuna pengo katika ufahamu sahihi wa Uislamu kutokana na kuwa kitabu hiki kitukufu kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu. Nilihisi kuwa kuna haja ya tarjama ya Qur’ani kwa lugha asili ya watu wa Magharibi mwa Kenya,” amesema Sheikh Musa.

Amesema tarjama hiyo ya Qur’ani itategemea lahaja za Kiwanga na Kimarama za lugya ya Kiluhya kwa sababu lahaja hizo haziegemei upande wowote na zinafahamika na watu wote Waluhya wenye lahaja 18 tafauti.

Wakizungumza wakati wa kuzinduliwa kazi ya tarjama hiyo siku ya Jumapili katika Msikiti wa Jamia wa Mumia, wasomi hao wamesema Waislamu wengi hawafahamu Qur’ani wakiisoma kwa Kiarabu na kwa msingi huo kuna haja ya tarjama kwa lugha asili.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Kadhi wa kaunti ya Kakamega Shaban Abu Issah, Kadhi wa Bungoma Kassim Ratori, Imam wa Msikiti wa Jamia wa Mumias Hamza Ismail and na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waislamu Ismail Muchelule.

Sheikh Issa amesema tarjama ya Qur;ani kwa Kiluhya mbali na kuwasaidia Waislamu pia itawafaa wasiokuwa Waislamu ili waufahamu Uislamu.

3486240

captcha