IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Nchi za Kiislamu zishirikiane katika vita dhidi ya ugaidi

23:07 - April 11, 2016
Habari ID: 3470242
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ili kupambana na hatari ya ugaidi na muamala wa kindumakuwili wa madola makubwa, kuna haja kwa nchi za Kiislamu kuongeza ushirikiano wao katika fremu ya siasa za kutimia akili na za kimantiki.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema hayo leo mjini Tehran katika mazungumzo yake na Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa amesema kuwa, Marekani na madola yanayodai kupambana na ugaidi hayana nia safi katika kukabiliana na tatizo hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kwamba, hatua ya Marekani ya kulisaidia kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq ni mfano wa wazi wa miamala isiyo na nia safi ya miungano mbalimbali inayodai kupambana na ugaidi. Amesema, madola hayo yakiwa na nia ya kuhalilisha miamala yao hiyo ya kindumakuwili yameugawa ugaidi katika sehemu mbili yaani ugaidi mzuri na ugaidi mbaya.

Kwingineko katika mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei amesisitiza udharura wa kuongezwa ushirikiano wa Iran na Kazakhstan katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, masuala ya kimataifa na vita dhidi ya ugaidi.

Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina hisia ya undugu na nchi za Kiislamu na misimamo ya Iran na Kazakhstan nayo inalingana katika masuala mengi.

Kwa upande wake Rais Nursultan Nazarbayev ameashiria uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nafasi ya kimaanawi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nchi za Kiislamu na kubainisha kwamba, anakubaliana kikamilifu na Kiongozi Muadhamu na mitazamo yake kuhusiana na umoja wa ulimwengu wa Kiislamu. Amesema, kuna haja ya kuuonesha ulimwengu wote kwamba, Uislamu ni dini ya maendeleo, umoja, na inayopambana na ugaidi.

3487758

Kishikizo: iran ، kazakhstan ، khamenei ، kiislamu ، ugaidi ، marekani ، iqna
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha