Inasemekana kuwa lori hilo liliendelea kuwakanyaga raia hao kwa masafa ya kilomita mbili huku dereva wake akiwafatulia risasi raia wengine waliokuwa karibu yake wakijaribu kuokoa maisha yao. Bernard Cazeneuve Wairi wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa ametangaza kuwa tayari watu wasiopungua 84 wamepoteza maisha yao na kuwa wengine 18 ni mahututi. Watu wengine 100 wamejeruhiwa katika tukio hilo la kigaidi lililotekelezwa katika mji wa kitalii wa Nice. Dereva wa lori hilo aliuawa na polisi ambao walipata kwenye gari hilo nyaraka zinazohusiana na raia mmoja wa Ufaransa aliye na umri wa miaka 31 mwenye asili ya Tunisia. Tokea shambulio jingine lililotekelezwa na magaidi mjini Paris tarehe 13 Novemba mwaka uliopita na jingine lililotekelezwa na magaidi wa Daesh mjini Brussels mwaka huu, shambulio la Nice ndilo shambulio kubwa zaidi la kigaidi kuwahi kutekelezwa nchini Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni. Inaonekana kuwa mfululizo wa vitendo vya ugaidi ungali unaendelea nchini Ufarsansa na hii ni katika hali ambayo Rais Francois Hollande wa nchi hiyo alikuwa ametangaza jana Alkhamisi juu ya uwezekano wa kuondolewa hali ya hatari nchini humo. Shambulio la hivi karibuni limethibitisha wazi kwamba viongozi wa ngazi za juu wa Ufaransa kidhahiri walikuwa na matumaini makubwa kupita kiasi kuhusiana na hali ya usalama ya nchi hiyo na ndio maana mara tu baada ya kutokea shambulio la hivi karibuni wameshtuka na kuchukua uamuzi wa kurefusha hali hiyo ya hatari kwa miezi mingine mitatu. Sambulio hilo linapaswa kuchunguzwa katika mtazamo wa mashambulio mengine ambayo yamekuwa yakiilenga Ufaransa tokea mwaka uliopita. Ni wazi kuwa shambulio hilo litakuwa na taathira kubwa katika mwenendo wa hatua za baadaye za kiusalama ambazo zitachukuliwa si tu na viongozi wa Ufaransa bali katika nchi zote za Ulaya na bila shaka hatua za hivi sasa za kiusalama katika nchi hizo zitabadilika sana. Kufuatia mashambulio ya Januari na Novemba mwaka uliopita wa 2015 nchini Ufaransa raia wa nchi hiyo walishuhudia mabadiliko makubwa ya sheria yakiwemo ya kupokonywa uraia wa Ufaransa watu wanaohusishwa na vitendo vya ugaidi, sheria ambayo ilikosolewa vikali kutokana na kuwalenga kidhulma watu walio na uraia wa nchi mbili nchini humo. Licha ya hayo lakini inaonekana kuwa mabadiliko hayo ya sheria na kutekelezwa sheria ya hali ya hatari hakujaweza kuzuia vitendo vya ugaidi katika ardhi ya nchi hiyo, jambo ambalo limezua maswali mengi kuhusiana na uwezo wa vyombo vya usalama vya nchi hiyo kuweza kukabiliana na ugaidi. Kwa kutilia maanani kwamba Daesh imetangaza kuhusiaka na shambulio la hivi karibuni la ugaidi huko mjini Nice, swali linaloulizwa hivi sasa ni kuwa je, ni kwa nini kundi hilo la kigaidi limeamua kutekeleza tena mashambulio ya ugaidi katika ardhi ya Ufaransa? Kuhusiana a mashambulio ya awali ya ugaidi, Daesh ilitangaza kuwa ilihusika nayo kutokana na Ufaransa kujiunga na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi yake huko Syria. Kwa hakika nchi za Ulaya na hasa Uingereza na Ufaransa ambazo ni wanachama muhimu wa Umoja wa Ulaya zikishirikiana na Marekani na washirika wao wa Kiarabu katika eneo la Mashariki ya Kati zimekuwa na nafasi muhimu katika kuunda na kuimarisha makundi ya kigaidi katika eneo na sasa zenyewe zimeanza kuonja matunda ya matendo yao hayo kwa njia mbili. Njia ya kwanza ni wimbi kubwa la wakimbizi wanaomiminika kwenye ardhi zao na ya pili ni mashambulio ya kigaidi yanayotekelezwa katika nchi hizo za Ulaya na raia wa nchi hizo zenyewe waliojiunga na kundi la kitakfiri na Daesh. Waulaya na hasa Wafaransa hawakudhani kwamba siku ingefika ambapo wangeanza kulipwa malipo ya matendo yao ya kubuni na kuyaimarisha makundi ya kigaidi huko Syria. Ukweli ni kwamba sasa nchi za Ulaya zimeanza kuvuna mavuno ya mbegu za ugaidi zilizopanda katika Mashariki ya Kati. Uzoefu unaonyesha kwamba baada ya kudhaminiwa na nchi za Magharibi, makundi ya kigaidi yenyewe ndiyo huwa na uamuzi wa mwisho kuhusiana na jinsi, sehemu na wakati wa kutekelezwa mashambulio ya kigaidi na hivyo kuzipokonya nchi hizo uwezo wa kuyaainishia majukumu. Hio ndio maana nchi hizo na hasa Ufaransa, licha ya kuchukua hatua kali za kiusalama lakini zimeshindwa kabisa kuzuia utekelezwaji wa vitendo vya ugaidi katika ardhi zao.