IQNA

Dr. Ahmed Omar Hashem, Rais wa zamani wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar na mwanazuoni mkuu, amefariki dunia

20:03 - October 07, 2025
Habari ID: 3481335
IQNA – Dr. Ahmed Omar Hashem, aliyewahi kuwa Rais wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar na mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wakuu wa taasisi hiyo, ameaga dunia alfajiri ya leo baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Ukurasa wake rasmi wa Facebook ulitangaza msiba huu kwa ujumbe uliosema: “Kwa nyoyo zilizojaa imani na taslim kwa qadha ya Mwenyezi Mungu, tunatangaza kifo cha mwanazuoni mtukufu Dr. Ahmed Omar Hashem … kwa ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, kwa wapendwa wake na wanafunzi wake.” Ujumbe huo uliomba daraja ya juu kwa marehemu na subira kwa waliopatwa na msiba.

Mazishi (salat al-janazah) yanatarajiwa kufanyika baada ya swala ya adhuhuri katika Msikiti Mkuu wa Al-Azhar. Baada ya swala ya alasiri, mwili wake utapelekwa kwenye kaburi la familia katika eneo la Hashimiyah, kijiji cha Bani Amer, karibu na mji wa Zagazig, katika mkoa wa Sharqia, Misri.

Dr. Hashem alizaliwa tarehe 6 Februari 1941. Mwaka 1961, alihitimu kutoka Kitivo cha Usul al-Din katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar. Alipata ijazah yake mwaka 1967, kisha akahudumu kama msaidizi wa kufundisha katika idara ya Hadith. Mwaka 1969, alipata shahada ya uzamili katika elimu ya Hadith, na baadaye shahada ya uzamivu katika fani hiyo hiyo. Kufikia mwaka 1983, aliteuliwa kuwa Profesa wa Hadith, na mwaka 1987 akawa Mkuu wa Kitivo cha Usul al-Din huko Zagazig. Mwaka 1995, aliteuliwa kuwa Rais wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar.

Zaidi ya taaluma, Dr. Hashem alishikilia nyadhifa mbalimbali za kiutawala na kisiasa. Alikuwa mbunge katika Bunge la Watu la Misri chini ya Rais Hosni Mubarak, mshiriki katika ofisi ya kisiasa ya Chama cha Kitaifa cha Kidemokrasia, na pia alikuwa mjumbe wa Baraza la Ushauri (Shura). Alikuwa pia mjumbe wa bodi ya Muungano wa Redio na Televisheni wa Misri na Mwenyekiti wa Kamati ya Vipindi vya Kidini katika televisheni ya taifa.

Kupitia vitabu vyake, tafiti, na ushiriki wake katika makongamano ya kimataifa ya Kiislamu, Dr. Hashem alitoa mchango mkubwa katika nyanja za Hadith na elimu ya dini. Baada ya kufufuliwa kwa Baraza la Wanazuoni Wakuu wa Al-Azhar mwaka 2012 (1433 Hijria), aliteuliwa kuwa mjumbe wake.

Katika ujumbe wake, Sheikh Mkuu wa sasa, Ahmed el-Tayeb, alimtaja marehemu kama “mamlaka halisi ya Al-Azhar na miongoni mwa wanazuoni wa Hadith mashuhuri wa zama zetu.” Alisisitiza fasaha yake, ikhlasi, na juhudi zake za kueneza elimu ya Kiislamu, akisema kwamba khutba zake, vitabu, na mihadhara yake vitabaki kuwa hazina kwa wanafunzi na watafiti.

Sheikh Ahmed el-Tayeb pia alitoa mkono wa pole kwa familia ya Dr. Hashem, wenzake, na wanafunzi wake.

“Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un. Mwenyezi Mungu amrehemu na ampe daraja ya juu peponi, na awape subira waliompoteza.”

3494912

Kishikizo: misri al azhar
captcha