IQNA

Mufti wa Misri

ISIS (Daesh) si Dola la Kiislamu

0:02 - October 07, 2016
Habari ID: 3470602
Mufti wa Misri amevitaka vyombo vya habari vya nchi za Magharibi viache kutumia neno "Dola la Kiislamu" kuliarifisha kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Sheikh Shouqi Alam amesema tangu hapo awali Idara ya Fatwa ya Misri (Darul Iftaa) ilitahadharisha kuhusu utumiaji wa neno 'Dola la Kiislamu' kama jina la kundi la kigaidi la ISIS. Mufti wa Misri ameongeza kuwa, vitendo vinavyofanywa na kundi la ISIS havipasi kunasibishwa kwa Waislamu na Uislamu na kwamba vyombo vya habari vya Magharibi vinapaswa kuacha mara moja kutumia neno "Dola la Kiislamu" kwa maana ya jina la kundi hilo. Mufti wa Misri amesisitiza kuwa, vyombo vya habari vinapaswa kuliita kundi hilo jina na taasisi ya kigaidi ya ISIS.

Sheikh Shouqi Alam amesema, kutumia neno Dola la Kiislamu kama jina la kundi la kigaidi la ISIS kunazusha tashwishi katika fikra za mataifa mbalimbali duniani kuhusu dini tukufu ya Uislamu. Ameongeza kuwa, kimsingi matendo na harakati za kundi hilo la kigaidi hazina mfungamano na uhusiano wowote na sheria za Kiislamu na kundi hilo kwa hakika ni genge la watenda jinai na magaidi. 

Matamshi hayo ya Mufti wa Misri yametolewa wakati Chuo Kikuu cha al Azhar mjini Cairo ambacho ndiyo kituo kikuu cha Waislamu wa madhehebu ya Sunni, katika miaka ya hivi karibuni kimetekwa na fikra za uwahabi, ambao ndio chimbuko na chemchemi ya misimamo mikali na ya kufurutu mipaka inayojenga msingi wa kifikra wa kundi la kitakfiri na kigaidi la ISIS.

Utawala wa Aal Saud ambao ni chimbuko halisi la fikra na idiolojia  ya Kiwahhabi ambayo inatumiwa na makundi ya kigaidi ya Kitakfiri kama vile ISIS, Al Qaeda, Al Shabab, Taliban na Boko Haram. Makundi hayo yanachochea machafuko na oparesheni za kigaidi huko Syria, Iraq, Lebanon, Yemen, Pakistan, Libya, Somalia, Nigeria na maeneo mengine mengi duniani. 

3535295


captcha