IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuwa na uhusiano na Marekani hakutatui matatizo ya nchi hata kidogo

20:59 - November 02, 2016
Habari ID: 3470648
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa moyo na fikra za kimapinduzi, ushujaa, ujasiri na uchapakazi, kuona mbali, ubunifu, kuwa na matarajio ya mustakbali mwema, kutoogopa na kutosalimu amri mbele ya adui vitatatua matatizo ya nchi hii.

Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran katika hadhara kubwa ya wanafunzi waliokwenda kuonana naye kabla ya maadhimisho ya siku ya tarehe 13 Aban (4 Novemba) ambayo ni Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa hapa nchini. Vilevile ametahadharisha kuhusu baadhi ya harakati na njama hatari zinazofanyika kwa shabaha ya kupotosha uhakika na mantiki ya kusimama kidete Imam Ruhullah Khomeini na taifa la Iran katika kupambana na Marekani katika fikra za kizazi cha vijana na kueneza dhana kwamba njia pekee ya utatuzi wa matatizo ya nchi hiyo ni kufanya mazungumzo na mapatano na Marekani. Kiongozi Muadhamu amebainisha zaidi kwa kusema: " Fikra ghalati inayohimizwa na Marekani, hata baadhi ndani ya nchi wanaieneza ni kuwa, iwapo tutakuwa na uhusiano mzuri na Marekani matatizo yetu yatatuliwa. Hili ni fikra hatari sana, ghalati na ni hadaa na uongo mtupu. Matatizo ya nchi kamwe hayawezi kutatuliwa kwa kuwa na uhusiano na Marekani bali hata matatizo yatakuwa mabaya zaidi."

Akiashiria matukio ya kihistoria ya siku ya tarehe 13 Aaban, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, tukio kubwa zaidi la siku hiyo ni kudhibitiwa Pango la Ujasusi(ubalozi wa Marekani mjini Tehran). Ameongeza kuwa, siku hiikwa hakika ni siku ya vijana wenye imani, wanamapinduzi nawabunifu ambao walibatilisha harakati za adui kwa kudhibiti pango hilo la ujasusi.

Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei amekumbusha hatua ya Imam Khomeini ya kutaja kitendo cha wanafunzi wa vyuo vikuu cha kudhibitiPango la Ujajusi (yaani ubalozi wa Marekani mjini Tehran) kuwa ni "Mapinduzi ya Pili" na akasema: Hatua hiyo ya Imam ni kutokana na njama na maovuyaliyofanywa na Marekani hapa nchini kabla na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya taifa la Iran, kwani serikali ya Marekani haikuacha kufanya jambo lolote rasmi na lisilo rasmi linalowezekana kwa ajili ya kuvunja na kuzima Mapinduzi ya Kiislamu; hivyoharakati ya vijana wanamapinduzi ya kudhibiti na kutwaa ubalozi wa Marekani katika kipindi hicho ilizima njama hizo.

Mdahalo wa Wagombea Urais Marekani

Baada ya hapo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria midahalo ya wagombea wawili wa kiti cha rais nchini Marekani na kusema: Katika siku hizi wagombea hao wawili wanafichua uhakika na maafa ya ndani ya Marekani ambayo awali baadhi ya watu hawakuamini kama yapo au hawakutaka kuamini hivyo; lakini hii leo matamshi ya wagombea hao wawili yanadhihirisha kutoweka kwa maadili ya kibinadamu nchini Marekani.

Akitoa ushahidi wa wagombea hao wawili kuhusu suala la ubaguzi wa rangi na kizazi, na umaskini nchini Marekani, na vilevile suala kuwa asilimia 90 ya utajiri wa Marekani unamilikiwa na asilimia moja tu ya watu wa jamii ya nchi hiyo, Kiongozi Muadhamu amesema: Kukanyagwa kwa maadili nahaki za binadamu, ukosefu wa usawa na ubaguzi wa kimbari ni miongoni mwa mambo ya hakika katika jamii ya sasa ya Marekani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taifa la Iran lilisimama kidete kupambana na Marekani katika kipindi cha hayati Imam Khomeini na hii leo bado linatoa nara dhidi ya Marekani na kusimama kidete dhidi ya nchi hiyo kwa kutumia mantiki na hoja zenye nguvu. 

Historia ya Aban 13 (Novemba 14)

Katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Aban 13 inajulikana kama Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari. Mnamo tarehe 4 Novemba ya mwaka 1964, 1978 na 1979 yalijiri matukio matatu muhimu katika historia ya Iran. Nukta ya pamoja katika matukio matatu hayo ni mapambano ya wananchi wa Iran ya kupigania kujitawala, uhuru na kujitoa kwenye makucha ya satua na ubeberu wa Marekani. Katika tukio la kwanza la mwaka 1964 Imam Khomeini alilazimishwa kuondoka nchini na kupelekwa uhamishoni Uturuki na hatimaye Iraq kwa sababu ya upinzani wake dhidi ya misimamo ya utawala wa Kifalme ya kujidhalilisha na kujidunisha mbele ya Marekani. Katika tukio la pili la tarehe 4 Novemba mwaka 1978 vikosi vya utawala kibaraka wa Shah viliwaua kwa kuwapiga risasi wanafunzi kadhaa mbele ya chuo kikuu cha Tehran. Na ama katika tukio la tatu lililojiri katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja baada ya Mapinduzi ya Kiislamu wanachuo wanaofuata miongozo ya Imam Khomeini waliuvamia na kuuteka ubalozi wa Marekani hapa Tehran na kukomesha ubeberu wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Washington katika nchi hii.

3542848

captcha