IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuendelezwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kinyume na mapatano ya nyuklia

23:01 - November 23, 2016
Habari ID: 3470694
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, hatua ya Marekani kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kwa miaka 10 zaidi, bila ya shaka yoyote ni uvunjaji wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesema hayo leo hapa mjini Tehran wakati alipoonana na makamanda wa jeshi la Basiji, na huku akigusia hatua ya Baraza la Kongress la Marekani ya kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi amesema kwamba, serikali ya hivi sasa ya Marekani imefanya ukiukaji mkubwa sana wa makubaliano ya nyuklia na miongoni mwake ni kurefushwa vikwazo hivyo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kama vikwazo hivyo vitatekelezwa kivitendo, bila ya shaka yoyote utakuwa ni uvunjaji wa makubaliano ya JCPOA na Wamarekani wajue kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itajibu jambo hilo.

Vile vile ameashiria matamshi ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na wasimamiaji wa makubaliano ya JCPOA ambao walisema kuwa, lengo la makubaliano hayo ya nyuklia ni kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran na kuongeza kuwa, makubaliano ya nyuklia yaani JCPOA hayapaswi kutumiwa kabisa kama mashinikizo dhidi ya taifa na nchi ya Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia masuala yanayozihusu Iran na serikali ya Marekani na kusema kuwa: Sisi hivi sasa hatuwezi kusema lolote kuhusiana na serikali mpya inayosubiriwa kuingia madarakani huko Marekani.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, Iran hailiogopi dola lolote duniani kutokana na imani  yake kwa Mwenyezi Mungu na kwa kutegemea nguvu za wananchi wake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amezungumzia kufanyika kwa mafanikio makubwa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS na kuongeza kuwa: Kushiriki mamilioni ya watu kwenye matembezi hayo kunaonesha mapenzi, mvuto pamoja na muono wa mbali walio nao maashiki hao wa Imam Hussein AS.

Ayatullahil Udhma Khamenei vile vile amewashukuru sana wananchi wa Iraq kwa kujitolea kwa mapenzi makubwa kuwahudumia wageni wa Imam Hussein AS na kutoa tahadhari akisema, kuna baadhi ya watu wana nia ya kuifuta na kuipotosha Arubaini ya Imam Hussein AS lakini hawatafanikiwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameashiria pia jinsi nchi nyingine za eneo hili zilivyochukua kigezo cha Basiji katika mambo yao mbalimbali na jinsi adui anavyofanya njama za kutoa pigo kwa kigezo hicho muhimu na kuongeza kuwa, moja ya njama za adui ni suala muhimu mno la kujipenyeza  ndani ya jamii ya Iran jambo ambalo nimekuwa nikilitolea tahadhari kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

3548197



captcha