IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Magaidi kama ISIS wametokana na uingiliaji wa madola makubwa katika eneo

21:34 - November 22, 2016
Habari ID: 3470691
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matukio machungu na ya kusikitisha katika eneo na nafasi ya baadhi ya madola makubwa katika kulazimisha ukosefu wa uthabiti na vita katika mataifa.
Kiongozi Muadhamu amesistiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitoa wito kwa nchi zenye misimamo huru kuwa na nafasi yenye harakati katika kukabiliana na mashinikizo dhidi ya mataifa na inayataka yasikae kimya na kuwa watazamaji."

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumanne alasiri mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Borut Pahor Rais wa Slovenia na ujumbe alioandamana nao ambao walikuwa safarani nchini Iran. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa mapigano yanayoendelea katika nchi za Magharibi mwa Asia na kuibuliwa makundi ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS) ni matokeo ya uingiliaji na ulazimishaji wa baadhi ya madola makubwa.

Ameongeza kuwa: "Ni jukumu la nchi zote kujitahidi kuzima moto wa machafuko na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kinyume na propaganda za madola ya kibeberu, inafuatilia lengo hili kivitendo na imekuwa na taathira na wala haiingilii masuala ya ndani ya nchi zingine."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema muungano wa Marekani dhidi ya Daesh haujafanikiwa. Katika kubainisha sababu za kutofanikiwa huko, ameashiria mitazamo miwili iliyopita na kusema: "Kwa mujibu wa mtazamo wa kwanza, Marekani haina mpango wowote wa kung'oa mizizi ya Daesh na inataka, kama ilivyokuwa Uingereza katika zama za ukoloni wake India, ilibakisha Kashmir kama kidonda kilicho wazi, na hivyo nchi mbili jirani za Pakistan na India hadi leo zinazozana. Kuhusu Daesh pia Marekani inataka tatizo hilo lisitatuliwa na libakie Iraq na Syria."

Kiongozi Muadhamu aliendelea kusema kuwa: "Kwa mujibu wa mtazamo wa pili, Marekani inataka kutatua  kadhia ya Daesh lakini kwa njia inazotumia haiwezi kutekeleza jambo hilo. Matokeo ya mitazamo hiyo miwili ni sawa kwani leo Iraq na hasa Syria iko katika hali chungu na ngumu sana."

Ayatullah Khamenei ameashiria matokeo ya kuibua machafuko katika nchi za Magharibi mwa Asia kuwa ni pamoja na tatizo la wakimbizi na kuongeza kuwa: "Katika hali ambayo nchi za Ulaya hazijaweza kuwapa hifadhi makumi ya maelfu ya wakimbizi, kwa muda wa miaka mingi sasa Iran imewapa hifadhi raia milioni tatu wa Afghanistan na kuwaandalia mazingira ya elimu na maisha bora na kuonyesha muamala bora zaidi wa kibinadamu kwa wahamiaji."

Kiongoziz Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua ya serikali ya Saudia kudondosha mabomu na kuharibu miundo msingi ya Yemen kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minane sasa na kutaja suala hilo kuwa moja ya matukio machungu katika eneo la Magharibi na Asia. Ameongeza kuwa: "Serikali zenye misimamo huru zinapaswa kukabiliana na suala hilo kwani kulishinikiza taifa moja ni sawa na uchungu na masaibu ya wanadamu wote."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria kuhusu namna ambavyo Iran imetekeleza ahadi zake  zote katika mapatano ya nyuklia na wakati huo huo akakosoa pande zingine za mapatano ambazo hazijatekeleza ahadi zao.

3548116


captcha