IQNA

Iran yalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya Mahakama ya ICC

23:59 - June 12, 2020
Habari ID: 3472860
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya Marekani kuwawekea vikwazo maafisa kadhaa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kusema, hivi sasa ICC inahujumiwa na genge la wahalifu wambao wanajiarifisha kuwa ni wanadiplomasia."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya Marekani kuwawekea vikwazo maafisa kadhaa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kusema, kitendo hicho cha Marekani ni ubabe na kuongeza kuwa hivi sasa ICC imehujumiwa na wahalifu na wakwepaji sheria ambao wanajifanya kuwa ni wanadiplomasia.

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo katika ujumbe alioandika katika ukurasa wake wa Twitter Alkhamisi usiku ambapo mbali na kulaani uamuzi huo wa Marekani amekosoa pia kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya utumiaji mabavu wa Marekani.

Katika ujumbe wake huo, Zarif ameandika: "Ni kipi kingine kinapaswa kutendeka ili jamii ya kimataifa iweze kufahamu madhara yanayotokana na kuridhia utumiaji mabavu."  Zarif ameendelea kuhoji, je, ni nani mwingine atahujumiwa na Marekani kabla ya wanaoridhia wafahamu ndio watakaolengwa?

Rais Donald Trump wa Marekani siku ya Alhamisi alitia saini dikrii ya vikwazo dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Trump amesema  hatua ya ICC kuazimia kufanya uchunguzi dhidi ya maofisa wa kijeshi na ujasusi wa Marekani waliohudumu Afghanistan unatishia mamlaka ya kujitawala, usalama wa taifa na sera za diplomasia za Marekani.

Wakati huo huo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imepinga vikwazo ilivyowekewa na Marekani na kuvitaja kuwa ni juhudi zisizokubalika katika utekelezaji sheria.

Mahakama hiyo iliyo na makao makuu yake mjini Hague Uholanzi imetoa taarifa  Ijumaa alfajiri ikisema kuwa vikwazo hivyo ni juhudi za hivi karibuni zaidi na zisizokuwa na mfano wake zinazofanywa na Marekani dhidi ya mahakama hiyo ya kimataifa.

Vyombo vya habari vya Marekani vimesema Afghanistan ni nchi mwanachama wa ICC, hivyo mahakama hiyo ina mamlaka ya kuchunguza uhalifu uliotokea nchini humo.

Mwezi Machi mwaka huu, majaji  katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) waliamuru uchunguzi uanze kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu ambazo zinaripotiwa kufanywa na askari wa Marekani nchini Afghanistan.

598532

captcha