IQNA

Qari chipukizi wa Iran aelezea safari yake ya kutambuliwa kitaifa

16:07 - November 05, 2025
Habari ID: 3481473
IQNA – Amirhossein Landarani, kijana mchanga wa Iran anayesoma na kuhifadhi Qur'an, ambaye hivi karibuni alishinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha usomaji wa mashindano ya 48 ya Kitaifa ya Qur'an nchini Iran, amesema mafanikio hayo ni miongoni mwa matukio yenye maana kubwa maishani mwake.

Landarani alizaliwa mwaka 2007, na alianza kuhudhuria vikao vya Qur'ani mjini Tehran akiwa na umri wa miaka mitatu, akihimizwa na baba yake pamoja na kaka yake mkubwa.

"Baada ya miaka minne ya kusikiliza na kujifunza pamoja nao, nilianza kusoma kwa ufanisi," aliambia IQNA. "Mwanzoni nilikuwa naiga mtindo wa Sheikh Abdul Basit, kisha nikabadilika na kufuata mtindo wa Sheikh Mustafa Ismail, ambao uliendana zaidi na sauti yangu."

Katika mashindano ya kitaifa yaliyoandaliwa na Taasisi ya Awqaf na Masuala ya Hisani ya Iran, Landarani alishinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha “Usomaji wa Tajweed” kwa walio chini ya miaka 18. Fainali ya mashindano hayo ilifanyika mwezi uliopita katika mkoa wa Kordestan, magharibi mwa Iran.

"Ushindi huu ulikuwa wa kipekee," alisema Landarani. "Ni tukio muhimu zaidi la Qur'ani nchini, na baada ya kushika nafasi ya pili mwaka jana, hatimaye juhudi zangu zimezaa matunda."

Aliongeza kuwa kushindana na wasomaji wakubwa waliobobea kulimpa maarifa ya kuboresha uwasilishaji wake.

Landarani alikamilisha kuhifadhi Qur'ani nzima tangu akiwa na umri wa miaka 13, na anasema uelewa wake wa maandiko umesaidia sana katika kuboresha ubora wa usomaji wake. Pia ni mwanachama wa kikundi cha vijana wasomaji wa Qur'an kilichoanzishwa chini ya Baraza Kuu la Qur'ani la Iran.

Mtindo wake wa sasa wa usomaji, anasema, umeathiriwa na ustadi wa Sheikh Mohammad Rif’at kutoka Misri.

Hivi karibuni, Landarani alichaguliwa kusoma Qur'ani katika mkusanyiko wa wanafunzi uliohudhuriwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo Novemba 3. "Nilipopata taarifa kuwa ningeanza hafla hiyo kwa usomaji, nilihisi furaha na wasiwasi kwa pamoja," alisema. "Lakini kwa baraka za Ahl al-Bayt (AS), niliweza kutoa usomaji mzuri. Huo ulikuwa miongoni mwa wakati bora kabisa maishani mwangu."

Kwa sasa akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Farhangian, Landarani anasema anataka kuendelea kujifunza na kuboresha. "Bado niko mwanzoni mwa safari hii," alisema. "Lengo langu ni kuiwakilisha Iran katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu."

3495269

captcha