IQNA

Bunge la Misri laafiki kutuma wanajeshi nchini Libya

21:58 - July 21, 2020
Habari ID: 3472984
TEHRAN (IQNA) - Bunge la Misri limeidhinisha wanajeshi wa nchi hiyo kutumwa Libya na hivyo kuandaa mazingira ya kuvamiwa kijeshi nchi hiyo jirani.

Kwa mujibu wa taarifa,Bunge la Misri Jumatatu lilifanya kikao cha siri na kumruhusu Rais Abdel Fattah el Sisi ya kutuma wanajeshi wa kupigana vita nje ya Misri.

Uamuzi huo wa Bunge la Misri umechukuliwa baada ya el Sisi kudai kuwa mgogoro wa Libya ni mstari mwekundu na kuna uwezekano serikali yake ikalazimisha kuingilia kijeshi mgogoro huo.

Alkhamisi iliyopita pia, rais huyo wa Misri alitishia kuivamia moja kwa moja kijeshi Libya kwa madai ya kulinda usalama wa kitaifa wa nchi zote mbili za Misri na Libya akidai kuwa, mji wa Sirte wa kaskazini mwa Libya na kambi ya jeshi la anga la Jenerali Khalifa Haftar iliyoko katikati ya Libya ni mstari mwekundu kwa Misri.

Matamshi hayo ya rais wa Misri yalikuwa ni vitisho vya kiwango cha juu kabisa kwa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa kimataifa.

Wakati huo huo Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan, ambaye anaunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya,  amekosoa hatua ya hivi karibuni za serikali ya Misri na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa jenerali muasi, Khalifa Haftar na kusema kuwa: Nchi yake itaisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya dhidi ya uvamizi wa Misri na kamwe haitawacha peke yao watu wa Libya. 

Itakumbukwa kuwa mwezi Disemba mwaka jana serikali ya Uturuki ilitia saini makubaliano na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya kuhusiana na ushirikiano katika Bahari ya Mediterania na kupanua ushirikiano wa kijeshi na kiusalama wa pande hizo mbili. Kufuatia matukio ya karibuni huko Libya, serikali ya Misri imetuma barua mbili tofauti kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Baraza la Usalama la umoja huo ikipinga rasmi makubaliano hayo. 

Tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kumng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi, Libya haijawahi kuwa na utulivu wa angalau hata siku moja. Uingiliaji wa madola ajinabi ndani na nje ya eneo hilo yanachochea zaidi mgogoro na ukosefu wa utulivu wa kisiasa na kiusalama nchini Libya.

3472049

Kishikizo: libya ، misri ، uturuki
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha