IQNA

Sudan yatuma wanajeshi Yemeni kupitia Saudia

21:21 - October 03, 2020
Habari ID: 3473227
TEHRAN (IQNA) -Baadhi ya duru za Saudi Arabia zimeripoti kuwa, wiki iliyopita Sudan ilipeleka mamia ya wanajeshi wake huko Yemen kupitia Saudia.

Duru hizi zinaeleleza kuwa, wiki iliyopita mamia ya wanajeshi wa Sudan waliwasili nchini Yemen wakipitia Saudia, hatua ambayo inaonyesha kuwa, serikali ya Khartoum imeongeza ushiriki wake katika vita nchini Yemen.

Mtandao wa Habari wa Middle East Eye umezinukuu duru za Saudia na kuandika: Wanajeshi 1,018 wa Sudan tarehe 22 Septemba waliingia Saudia kwa boti na kuvuka mpaka kupitia idara ya uhamiaji ya mji wa Jazan ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo na kuingia nchini Yemen.

Gazeti la al-Quds al-Arabi linaripoti kuwa, ndege mbili za Sudan pia ziliwasafirisha wanajeshi wa Sudan kutoka Khartoum hadi katika Uwanja wa Ndege wa Najran wa kusini mwa Sudan ambapo ndege ya kwanza ilikuwa imebeba wanajeshi 123 huku ya pili ikiwa na askari 128.

Imebainika kuwa, ndege hizo zilibeba askari na maafisa wa kijeshi ambao wamepelekwa nchini Yemen kwa ajili ya kushiriki katika operesheni ya "Kuhuisha Matumaini".

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Januari mwaka huu Sudan ilitangaza kuwa, inakusudia kupunguza idadi ya wanajeshi wake huko nchini Yemen kutoka 5,000 hadi 650.

Itakumbukwa kuwa, huko nyuma Sudan imewahi kutuma askari 15,000 nchini Yemen katika kalibu ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na dola vamizi la Saudia, muungano ambao hadi sasa umefanya mauaji makubwa na kuisababishia nchi hiyo masikini hasara kubwa hasa miundombinu ya nchi hiyo.

Katika maandamano yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Omar al Bashir mwaka 2019, wananchi wa Sudan walitaka askari wa nchi hiyo waondoke katika muungano wa kivita wa Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabi dhidi ya Yemen.

3472709/

Kishikizo: sudan yemen saudia vita
captcha