IQNA

Waziri Mkuu wa Yemen

Kufutwa Saudia katika orodha ya wanaokiuka haki za watoto ni doa katika uso wa Umoja wa Mataifa

16:35 - August 12, 2020
Habari ID: 3473060
TEHRAN (IQNA) - Waziri Mkuu wa Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa ya Yemen amekosoa hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuiondoa Saudi Arabia katika orodha ya wauaji wa watoto.

Abdulaziz Saleh bin Habtoor, Waziri Mkuu wa Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa nchini Yemen ameyasema hayo leo Jumatano wakati alipokutana na  Lise Grande Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Kibinadamu nchini Yemen na kuongeza kuwa: "Kufutwa jina la Saudia katika orodha ya wanaokiuka haki za watoto ni doa katika uso wa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa na hatua hiyo ni sawa na idhini kwa wavamizi kuendelea na mauaji yao ya umati dhidi ya watoto na wanawake nchini Yemen."

Bin Habtoor amekosoa baadhi ya taasisi za kimataifa nchini Yemen na kusema taasisi hizo ambazo zinadai kutoa misaada ziko nchini humo huku maafa ya maafa ya kibinadamu yakiendelea kushadidi na wakati huo huo mashambulizi ya muungano wa Saudia yanaendelea sambamba na mzingiro dhidi ya watu wa Yemen.

Wiki iliyopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa ripoti kuhusu watoto na vita katika mwaka 2019 na kusema muungano wa kivita wa Saudia umehusika katika mauaji ya watoto 222 nchini Yemen mwaka 2019 lakini pamoja na hayo akatoa jina la Saudiakatika orodha ya umoja huo ya wanaokiuka haki za watoto.

Mwaka 2017 Umoja wa Mataifa uliiweka Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wauaji na wakiukaji wakubwa wa haki za watoto kutokana na mauaji ya maelfu ya watoto wa Yemen na kuharibiwa shule na mahospitali ya nchi hiyo katika mashambulizi ya Saudia.

Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen. 

Mwezi Juni, Kituo cha Haki za Binadamu cha Ainul Insaniya kilitoa ripoti na kutangaza kuwa tokea muungano wa Saudia uanzishe vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 26, 2015 hadi sasa watu 16, 672 wamepoteza maisha moja kwa moja kutokana na vita ambapo miongoni mwao kuna watoto 3,742 na wanawake 2,364.

3916216

captcha