Fawzi Barhoum, Msemaji wa Harakati ya Mapambabno ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kitendo hicho cha Sudan ni hatua moja mbele kuelekea katika mkondo ghalati na uliojaa makosa.
Naye Abu Youssef, mwanachama wa Kamati Kuu ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema tangazo hilo la kuanzishwa uhusiano baina ya Khartoum na Tel Aviv katu halitayumbisha moyo na ari ya Wapalestina ya kuendeleza jitihada zao za ukombozi.
Wakati huo huo, makundi mawili muhimu ya kisiasa ya Sudan ya al-Muutamir na al-Baath sanjari na kulaani usaliti huo wa serikali ya Khartoum, yametoa mwito wa kuanzisha mrengo mmoja wa kitaifa wa kupinga kuanzishwa uhusiano wa nchi yao na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Huku hayo yakiarifiwa, Mufti Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmad bin Hamad Al-Khalili amekosoa vikali kitendo hicho cha baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni sawa na kupigwa tena jambia kwa nyuma Wapalestina.
Kadhalika Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa taarifa na kusema kuwa, hatua ya tawala vibara zinazojikomba kwa Marekani na Israel imetokana na tamaa na ubinafsi wao, na kwamba inasikitisha kuona baadhi ya watawala watenda jinai wanaipiga mnada kadhia tukufu na muhimu zaidi katika umma wa Kiislamu. Ansarullah imebainisha kuwa, watawala vibaraka wa Kiarabu waliotangaza bai'a kwa Marekani na utawala wa Kizayuni kamwe hawatapata ridhaa ya wananchi wanaowatawala, na hatua yao hiyo haitakuwa na natija isipokuwa fedheha na hasara.
Jana Ijumaa, Rais wa Marekani Donald Trump huku akizungumza kwa jeuri na majigambo alitangaza kuwa Tel-Aviv na Khartoum zimeafikiana kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao, na eti kuna nchi nyingine tano za Kiarabu zenye azma ya kufuata mkumbo huo. Sudan inakuwa nchi ya tatu ya Kiarabu baada ya Imarati na Bahrain kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, licha ya pingamizi na malalamiko ya wananchi wa nchi hizo na ulimwengu wa Kiislamu.