IQNA

Mwanachama mashuhuri wa chama cha Ennahdha akamatwa Tunisia

18:30 - August 07, 2021
Habari ID: 3474167
TEHRAN (IQNA)- Afisa mwandamizi wa chama cha Kiislamu cha Ennahdha nchini Tunisia anashikiliwa kifungo cha nyumbani kutokana na kile ambacho kimetajwa ni kutumia vibaya madaraka.

Anouar Maarouf ni mwanachama mashuhuri zaidi wa chama hicho kulengwa tokea Rais Kais Saied wa nchi hiyo alipomfuta kazi waziri mkuu na kusimamisha bunge kwa muda mnamo Julai 25 katika hatua ambayo ilitajwa na Ennahdha kuwa ni mapinduzi baridi.

Chama cha Ennahdha kimetoa taarifa na kusema Maarouf alifahamishwa Ijumaa na maafusa wa usalama kuwa yuko katika kifungo cha nyumbani lakini hakuonyeshwa amri yoyote ya kisheria iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Chama hicho kinasema uamuzi huo unakiuka haki yake ya kutembea na uhuru wa maoni.

Maarouf alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia mwaka 2016 hadi 2020. Rais Saied ameashiria kwa njia ya moja kwa moja kuwa wizaray hiyo ilitumiwa vibaya na vyama vya kisiasa.

Ingawa hatua ya mwezi jana ya Rais Saied inaonekana kuungwa mkono na wananchi lakini imeibua maswali mengi kuhusu mchakato wa kidemokrasia katika nchi hiyo ambayo ilikuwa ya kwanza kushuhudia mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu mnamo mwaka 2011.

Wanasiasa kadhaa hadi sasa wamefunguliwa faili za uchunguzi kuhusu makossa mbali mbali wanayodaiwa kuyatenda.

3475450/

Kishikizo: tunisia ennahdha saied
captcha